Makala

Umaskini unavyochangia ongezeko la wizi wa mifugo na mazao Mlima Kenya

Na MWANGI MUIRURI June 22nd, 2024 2 min read

KUONGEZEKA kwa umasikini kumezidisha wizi wa mifugo na mazao katika eneo la Mlima Kenya unaotishia kutumbukiza eneo hilo katika ukiukaji wa sheria huku wakulima wakigeukia kuchukua sheria mikononi mwao kwa kuua washukiwa wakilaumu idara za usalama kwa kutouzuia.

Mazao yanayolengwa ni parachichi, kahawa, chai, ndizi, muguka, maembe, mapapai, makadamia, nyanya, mboga na miwa huku mifugo kama ng’ombe, punda, mbuzi, kuku, sungura na nguruwe wakilengwa zaidi.

Wizi huo haujasaza hata kampuni za kimataifa kama kampuni ya mananasi ya Del Monte, ambayo imeitaka serikali kusaidia kuepuka hasara ya Sh50 milioni kwa mwezi inayosababishwa na magenge wanaovamia shamba lake la Murang’a kila siku.

Hali ni mbaya sana hivi kwamba inakadiriwa wizi wa mifugo na mazao eneo la Kati unakadiriwa kuchangia wastani wa asilimia 71 ya uhalifu wote ambao uliripotiwa katika eneo hilo katika mwaka wa kifedha wa 2022/23.

Bw Kanene Kabiru ambaye ni mkaguzi wa hesabu katika Rwathia Distributors, alisema “babu na baba zetu waliungana vijijini na kukusanya rasilimali ambazo zilipatikana kupitia biashara ya mifugo na mazao. Walitumia pesa hizo kuwekeza Nairobi na miji mingine mikuu. Inasikitisha kwamba uzalishaji vijijini unapungua kutokana na wakulima kuachana na biashara za jadi kutokana na wizi na hivyo kuwafanya wawe na kiasi kidogo cha fedha yaani umaskini.”

Bw Kabiru anasema ikiwa sekta za mifugo na mazao zingesimamiwa ipasavyo, “Mlima Kenya ungeafikia matarajio ya Ruwaza ya 2030 ndani ya miaka miwili.”

Mazao kama mananasi, maparachichi, kahawa, ndizi, chai yanavamiwa sana

Huku tishio hilo likiendelea kujadiliwa na wakulima wakiendelea kupoteza mifugo au mazao ya shambani kwa wezi, maafisa wa usalama wa eneo hilo wanaendelea kutoa ahadi baada ya ahadi.

“Ni kweli kwamba tuna changamoto hii ya usalama na kama kamati ya usalama ya eneo tumeidhinisha hatua mahususi za msingi kutusaidia kukabiliana na changamoto hiyo. Tumeunda kamati za usalama ambazo zimepewa jukumu la kuangamiza wizi huo,” alisema Kamishna wa eneo la Kati Fred Shisia.

Bw Shisia alisema, “tayari tumeongeza doria na tumekuwa na operesheni kadhaa ambazo zimetufanya kurejesha mazao ya shambani na mifugo iliyoibwa. Tunajua kuna kazi ya kufanywa na ninaahidi inafanywa.”

Mnamo Mei 2023, Waziri wa Mambo ya Ndani Kithure Kindiki alitangaza wizi wa mifugo na mazao kama changamoto eneo hilo na akaamuru vikundi viundwe ili kukabiliana na tishio hilo.

Akihutubia mkutano wa usalama Igembe Kaskazini baada ya aliyekuwa MCA wa wadi ya Antubetwe Kiongo, George Kaliunga kuuawa na watu wanaoshukiwa kuwa wezi wa mifugo, Waziri alisema lazima serikali ichukue hatua kali zaidi kukabiliana na tishio hili.

Mkuu wa polisi katika kaunti ndogo ya Ruiru Bw Alexander Shikondi aliambia Taifa Leo kwamba wizi wa mazao na mifugo unashamiri kwa kuwa kuna soko lililo tayari linalothibitiwa na mabwanyenye na mabroka.