Umbali kuwekwa makombe yakisherehekewa Ulaya

Umbali kuwekwa makombe yakisherehekewa Ulaya

 CHRIS ADUNGO

RB Salzburg waliwaponda Austria Lutenau 5-0 na kutwaa ubingwa wa OFB Austrian Cup katika ushindi ambao kikawaida, ungalishuhudia mbwembwe na mihemko ya kila sampuli miongoni mwa wachezaji na mashabiki wa wafalme wa taji hilo.

Hata hivyo, wakati ambapo soka imerejelewa chini ya masharti makali katika juhudi za kudhibiti maambukizi zaidi ya ugonjwa wa Covid-19, ushindi wa Salzburg haukushuhudiwa na mashabiki uwanjani wala tukio la mashabiki kujitoma vichochoroni kusherehekea mafanikio ya kikosi chao.

Licha ya wachezaji kukabiliana kwa karibu sana uwanjani kwa dakika 90 na hata kwa wakati fulani kushikana wakiwania mipira ya kona, mipango kabambe iliwekwa kuhakikisha kwamba wanasoka wa Salzburg hawakaribiani sana walipokuwa wakifurahia ufalme wao baada ya kutawazwa mabingwa.

Masogora hao wa kocha Jesse Marsch walilazimika kusimama kwenye mkeka mkubwa uliokuwa na michoro ya maumbo ya mviringo yaliyobainisha mahali ambapo kila mchezaji alistahili kusimamia ili kudumisha umbali wa hadi mita moja kati yao.

Nahodha Andreas Ulmer alipata fursa ya kunyanyua kombe katika uwanja mtupu wa Worthersee bila mashabiki.

Mtindo wa kusherehekea ubingwa kwa namna hiyo huenda sasa ukaigwa na vikosi vyote vinginevyo barani Ulaya hasa ikizingatiwa kwamba mengi ya mapambano yaliyokuwa yamesimamishwa yanarejelewa mnamo Juni 2020.

Taswira kuhusu yaliyotokea ugani Worthersee huenda ikashuhudiwa pia uwanjani Wembley, Uingereza siku ya kutawazwa kwa mabingwa wa Kombe la FA mnamo Agosti 1.

Hali sawa na hiyo huenda pia ikawakabili Liverpool ambao wanapigiwa upatu wa kutwaa ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya miaka 30.

  • Tags

You can share this post!

Je, Kenya ni taifa la wanariadha wapenda pufya?

Barca kukutana na Mallorca Juni 13

adminleo