Makala

UMBEA: Changamoto za kunyoosha viungo na mwenzako kazini

September 14th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

INGAWA mapenzi hayana macho, hayasikii na wala hayaoni, kuna hali zingine huwa zinaleta utata katika mahusiano.

Hivi majuzi nilishuhudia dada mmoja akikosa amani kazini baada ya uhusiano wake na mfanyakazi mwenzake kutumbukia nyongo. Kwamba alipendana na mwanamume wanayefanya kazi ofisi moja na uhusiano wao ulipofika kikomo, akajikuta anapata mateso moyoni.

Wengi wetu huwa tunatumia sehemu kubwa ya maisha yetu kazini ama katika shughuli tunazofanya kujikidhi kiuchumi.

Mazingira haya ya kazi, wakati mwingine, yanatengeneza uwezekano wa uhusiano wa kimapenzi baina ya wafanyakazi.

Kawaida unapokuwa na mtu mnayefanya naye kitu kinachofanana kwa muda mwingi, ni rahisi kuanza kuvutiwa naye.

Kadri mnavyoonana mara kwa mara ndivyo mnavyozidi kufahamiana kwa karibu. Hisia za mapenzi zinaweza kuzaliwa kama tahadhari hazitachukuliwa.

Ni dhahiri ofisi zinakutanisha watu wenye uelewa usiotofautiana sana, wenye mtindo wa maisha usiotofautiana sana na hivyo kuongeza uwezekano wa mahusiano ya karibu.

Vyovyote iwavyo, unapokuwa na mpenzi kwenye eneo la kazi, ni vigumu kuficha. Ingawa inategemea na ukomavu wenu, ni suala la muda tu kabla hamjaanza kuonekana karibu kuliko ilivyo kawaida. Tetesi zitakapoanza kuenea kwamba ‘mnatoka’ hamtazifurahia na zinaweza kutengeneza ufa baina yenu na wafanyakazi wenzenu.

Pia, wafanyakazi wenzenu kwa kutambua mapenzi yenu wanaweza kuanza kuwapa nafasi ya kuwa na faragha yenu wenyewe. Hali hii mtaitafsiri kama kutengwa na kuonewa wivu. Katika mazingira kama haya, ni rahisi uhusiano wenu na wafanyakazi wengine kuzorota.

Changamoto iliyopo ni kwamba unapokuwa na uhusiano na mfanyakazi mwenzako, unajiweka kwenye mitihani ya utendakazi.

Fikiria, kwa mfano, mazingira ambayo mmoja wenu kati ya nyinyi mlio wapenzi anawajibika kwa mwenzake kikazi. Kibinadamu ni vigumu kuacha kukupendelea. Katika mazingira ambayo wafanyakazi wengine wanashuhudia hilo likiendelea, sifa na maslahi ambayo pengine mmoja wenu angestahili kwa haki, inaweza kuibua maneno yatakayowaudhi.

Kwa upande mwingine, aliye chini ya mwenzake naye anaweza kuanza kuwa mzembe kazini akiamini mpenzi wake ambaye ndiye bosi atamlinda. Hali kama hii inaweza kuibua changamoto kubwa ya utendakazi.

Mkubwa ataanza kujisikia kudharaulika, na aliye chini ataanza kujisikia hatendewi haki pale atakapokosa kile anachokihitaji.

Yote tisa, kumi ni pale inapotokea tofauti baina yenu na halafu muone kuna umuhimu wa kukomesha uhusiano wenu. Ni wazi kwamba mapenzi yana nyakati zake ngumu pia.

Si mara zote unapoanzisha uhusiano na mtu mnaweza kuendelea kuwa wapenzi kwa muda mrefu. Inawezekana mkashindwa kuelewana kwa sababu moja au nyingine na mkaamua kuachana.

Hatari ya ugomvi wa mapenzi

Ugomvi wa mapenzi mara nyingi hufanya watu waliokuwa wapenzi wasiendelee kuwa marafiki.

Fikiria namna utakavyoendelea kufanya kazi na mtu ambaye alikufahamu kwa karibu sana na baadaye mkaachana.

Hali hii inaweza kusababisha kuzorota kwa kazi zako, utoro kazini na hata kuchukia kazi bila sababu za msingi. Kinachosababisha yote haya ni kuanza kuyahusisha mazingira ya kazi na mazingira ya ugomvi wenu wa kimapenzi. Katika mazingira kama haya, ni rahisi kupoteza utoshelevu kazini.

Mbali na kuathiri mawasiliano yako na wafanyakazi wenzako, mapenzi kazini yanaweza kukuingiza kwenye matatizo. Kumbuka kwamba maisha ya ofisini hayatoshi kumfahamu mtu. Unayefikiri anatafuta mwenza, inawezekana ameacha familia nyumbani. Uhusiano wa namna hii unaweza usiwe na mwisho mzuri.

Kifupi ni kwamba uhusiano kazini una changamoto nyingi zaidi kuliko faida zake. Hivyo unapoamua kunyoosha viungo na mfanyakazi mwenzako, kumbuka yanayoambatana na uamuzi wako.

 

[email protected]