Makala

UMBEA: Eti kuna aina tatu za wanaume; mwindaji, mla mizoga na mkulima!

May 22nd, 2020 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

NIMEDOKEZEWA kwamba kuna aina tatu kubwa za wanaume huku Uswahilini ninakoishi.

Na mimi ni nani nipinge, nikachukua jukumu la kuzungumza na akina kaka na akina dada kuhusu hayo niliyodokezewa na kwa uelewa wangu, ningependa kuwashirikisha pia.

Kuna wanaume ambao nimeambiwa wana hulka ya wawindaji. Na kawaida ya mwindaji hupenda kupata mnyama aliyenona, anayevutia, mwenye hadhi na mwenye sifa. Lakini tatizo kubwa la hawa wawindaji wanapopata kitu konki, kitu mubashara, wanaingiwa hofu na kutishwa na hilo windo ambalo limepatikana. Na ndiyo maana wanaume wa aina hii ni lazima wasambaratishe kwanza windo lao.

Hawa ndio wale wanaosaka na kuwinda wanawake waliofanikiwa kimaisha, wakateka nyoyo zao kimapenzi, kisha kuua kabisa ndoto zao, wataua urembo walio nao, kwani wanatishwa na urembo wa hilo windo. Na ndipo hapa utamsikia mwanamume akimwambia mpenzi ama mkewe, usipake hiyo rangi ya mdomo unaonekana kama bundi, usivae hilo gauni linachoresha mwili wako vibaya, usifanye hivi ama usifanye vile.

Halafu kuna wale wanaume wala mizoga, vitu vilivyochoka au viporo, hawana hulka ya uwindaji. Wanaume wa aina hii husaka mwanamke asiyejiamini, aliyejawa na woga na asiyeweza kujieleza na kutetea anachoamini. Husaka wanawake waliosambaratika kihisia, wale wanaohitaji sana kupendwa, wanaohitaji kuhudumiwa. Mwanamume wa aina hii hupenda wanawake wadhoofu, walio na mahitaji.

Hawa ndio wale wanaopenda kutembea na wanawake wenye uwezo mdogo wa kutathmini mambo, ama wanafunzi ambao hawana uzoefu wa kutetea wanachoamini, hawa ndio wale pia walio wataalam katika kutembea na wasichana wa kazi. Hivyo ukimuona mumeo ananyemelea wasichana wa kazi mara kwa mara, utambue kwamba umeolewa na muwinda mizoga.

Wapo wanaume ambao ni wakulima… Ndio wakulima wa bustani. Mwanamume wa aina hii ni yule anayeoa mwanamke na kumtunza kama vile unavyopanda mbegu kwenye udongo wenye rotuba. Kwani anapoamua kuishi naye, anajua kwamba mkewe anao uwezo mkubwa wa kuwa mkubwa kuliko alivyo wakati wanapoanza maisha ya ndoa. Anaona uwezo wake katika elimu, biashara, familia na mengine ambayo yanaweza kukuza na kuleta ushamiri wa maisha ya familia. Anampanda mkewe katika moyo wake na katika nyumba yake na kisha anammwagilia maji na kuweka mbolea ili aweze kushamiri na kukua zaidi na zaidi.

Hivyo kaka kama unashindwa kumfurahia mkeo, jiulize wewe ni mume wa aina gani. Je, ulianzisha uhusiano kwa lengo maalum la kupata mtu wa kutatua shida zako? Kwamba unajidai unampenda huyo mkeo, lakini moyoni kwako unatambua kabisa huna mpango naye.

Nawe msichana ukadhani umepata. Ukawekeza mapenzi yako yote ukiamini anafaa kuwa mwenza wako wa maisha. Lakini kumbe mwenzako hakupendi isipokuwa anajidai anakupenda ili akuchune tu.

 

[email protected]