Makala

UMBEA: Furaha hutoka moyoni, huwa hainunuliwi au kulazimishwa

July 5th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

MAISHA ni safari ndefu na katika safari hiyo ni muhimu kujielewa na kutambua aina ya maisha unayoishi.

Kichocheo cha muhimu katika maisha ya kila siku ni afya ya akili yako, unaishi kwa furaha ama unaishi kwa karaha?

Kutokana na changamoto za kimazingira, kiuchumi na kijamii, baadhi ya watu wamejikuta wakikosa furaha. Ni wazi kuwa kukosa furaha kuna madhara kwenye afya ya mwili, akili na hata katika utendaji wako wa kazi.

Wapo wengine hutamani kuwa na furaha lakini bado hawapati furaha, wengi hudhani kuwa na pesa ndiyo chanzo cha furaha, lakini mambo hayawi kama walivyotarajia pindi wapatapo hizo pesa.

Furaha hutoka moyoni na huwa hainunuliwi wala kulazimishwa. Ili uwe na furaha, huna budi kuamua kwamba unataka uwe na hali hiyo. Unaweza kuanza safari ya kuelekea kwenye furaha kwa kufanya yafuatayo:

• Samehe

Unapobeba uchungu, lawama na maumivu moyoni mwako ni nadra kuweza kuwa na furaha. Unapobeba taswira za watu waliokukosea na kuendelea kuishi nayo kwa muda mrefu, furaha utaisikia kwa wenzako. Ikiwa unataka kuwa na furaha, ni muhimu umsamehe aliyekukosea hata kama hajaomba msamaha.

Kumsamehe aliyekukosea kuna manufaa kwako zaidi kuliko kwa yule aliyekukosea. Mara nyingi aliyekosea huendelea na maisha yake ya kawaida huku aliyekosewa akizidi kuumia.

• Fanya unachokipenda

Mafanikio siyo ufunguo wa furaha. Furaha ni ufunguo wa mafanikio. Kama unapenda unachokifanya, utafanikiwa.

Moja kati ya siri ya kufanikiwa na kuwa na furaha katika kile unachokifanya ni kwa kupenda kile unachokifanya. Unapopenda kile unachokifanya, utakuwa na amani na furaha mara ukutanapo na changamoto au vikwazo.

• Kuwa na shukrani

Mara nyingi tunatazama mambo mengi kiasi cha kushindwa kuwa na shukrani kwa yale tuliyonayo. Ni rahisi kuona kuwa mambo kama vile afya, marafiki, usalama ama makazi ni mambo madogo ambayo hatupaswi kushukuru kwa ajili yake.

Kwa hakika wapo watu wanaotafuta mambo hayo lakini hawayapati. Hivyo ili kupata furaha ni muhimu kutambua na kushukuru kwa yale machache tuliyonayo.

• Saidia wengine

Kumsaidia mtu mwingine siyo kumpa pesa au vitu. Hata kumpa mtu ushauri au kumtia moyo kunaweza kuwa na maana kubwa kwa mtu huyo. Unapomsaidia mtu mwingine, unajisikia kuwa na thamani na furaha kwani umeweza kufanya kitu chenye manufaa kwenye maisha ya mtu mwingine.

• Shirikisha wengine

Inawezekana jambo linalokukosesha furaha kuna mtu mwingine anafahamu utatuzi wake. Hivyo kwa njia ya kumshirikisha mwingine utapata ushauri au hata utatuzi wa tatizo lako. Jambo la kuzingatia ni kuhakikisha unamshirikisha mtu sahihi.

• Ondoa mawazo hasi

Mawazo gani uliyonayo kwenye fikra zako? Je, unawaza tu huwezi au kushindwa? Mawazo hasi au ya kushindwa ni chanzo kikuu cha kukukosesha furaha.

Amini unaweza hata kama unaona giza. Leo ni giza, kesho ni mvua lakini keshokutwa jua litawaka. Fanya kazi na juhudi ya kufikia lengo lako.

Usikate tamaa, ondoa mawazo mabaya yanayokufanya ukose furaha na amani.

• Usitafute ukamilifu

Mara nyingi watu hukosa furaha kwa sababu wanatafuta ukamilifu. Kwa hakika hakuna binadamu aliyekamilika, wote tuna udhaifu na mapungufu ya aina mbalimbali.

Badala ya kutafakari udhaifu wako na kuruhusu ukukoseshe furaha, ukubali na ukabiliane nao kwa namna bora zaidi.

• Kaa na watu wanaochangia kuimarika kwako

Je, umezungukwa na watu wanaokulaumu, kukudharau au kukubeza kila wakati? Au pengine umekaa katikati ya watu walioshindwa na wanaolaumu na kulalamikia kila kitu?

Watu wa aina hii wanakusababisha ukose furaha. Hakikisha unakaa katikati ya watu wanaokutia moyo na kukuthamini. Epuka watu walioshindwa ambao kazi yao kubwa ni kulalamika na kulaumu kila kitu.

 

[email protected]