UMBEA: Hakuna mpenzi mzuri au mbaya inategemea tu ikiwa mnafaana

UMBEA: Hakuna mpenzi mzuri au mbaya inategemea tu ikiwa mnafaana

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA kawaida dunia sio mbaya, isipokuwa wanadamu ndio wabaya.

Na kwa dhana hii wapo akina dada ambao daima huamini kwamba hakuna mwanaume mzuri. Kwamba wanaume wote ni wabaya, tabia zao hazifai na tena mienendo na dhamira zao hufanana.

Kwa upande mmoja nitakubaliana nao, lakini pia kwa upande mwingine sitakubaliana nao.

Hakuna mtu anayezaliwa na ubaya, bali mazingira na maisha tunayokulia huchangia kwa kiasi kikubwa kutathmini maisha yetu ya baadaye tunapoingia katika uhusiano na hatimaye ndoa.

Wengi wetu tunapokua huwa tunakutana na mambo mengi. Yapo mazuri na mabaya pia. Na kawaida ya binadamu ni kukumbuka yale ambayo sio mazuri kwa urahisi zaidi kuliko yale ambayo ni mazuri.

Miongoni mwa hoja ambazo zinawakosesha raha baadhi ya wanawake, furaha na amani mioyoni mwao, hasa katika upande wa mapenzi ni kuamini kuwa, kuna mwanamke mzuri na mbaya.

Wapo baadhi ya wanawake ambao wamekuwa wakijishuku kuwa inawezekana dhana hiyo ndiyo chanzo cha wao kuachwa na wanaume wanaokuwa nao.

Inawezekana pia kuna mwanamke amewahi kusikia kwa mtu au amekuwa akisimangwa na mpenzi wake kuwa yeye ni mbaya wa sura na maumbile hivyo kumkosesha amani maishani mwake. Na wapo wale ambao wamekuwa wakisimangwa kwamba wana roho mbaya zilizotawaliwa na kutu.

Vivyo hivyo, kwa wanaume, wapo wanaohangaika huku na kule kutaka apate mwanamke mzuri wa maumbile huku akiamini labda aliye naye ni wa kawaida au si mzuri.

Hii ni dhana ambayo imeziteka fikra za wengi, kwa kuamini kuwa inawezekana aliyenaye si mwanaume au mwanamke mzuri.

Labda msomaji hujui hii, kuwa, hakuna mwanaume au mwanamke mzuri au mbaya. Isipokuwa mwanaume au mwanamke mzuri ni yule ambaye mnaendana, mnaelewana, mnaridhiana na mnaridhishana mnapokuwa faragha.

Ninasema hivyo kwa sababu uzuri ambao unasemwa na kufikiriwa na walio wengi ni uzuri usioweza kusikika, kuhisika, kushikika au kuhadithika.

Mapenzi ni hisia ambayo moyo huitaka kutoka kwa mwanamke au mwanaume husika. Ndiyo maana unaweza kuwa na mpenzi, ukaachana naye kwa mbwembwe nyingi kwa kuamini kuwa si mwanamke au mwanaume anayestahili kuishi na wewe wala mpenzi mwingine yeyote kwa sababu hana uzuri ambao uliufikiria, lakini mwisho wa siku wewe ukaangukia kisogo na mwenzako akafanikiwa kuwa na maisha mazuri ya mapenzi kuliko wewe.

Kuna wakati mwingine unaweza kumuona mpenzi uliyenaye ni mbaya, lakini wakati huohuo kuna mwenzako pale ndiyo kwenye pumziko la moyo wake. Yuko tayari kufanya jambo lolote ilimradi asimuache aende au awe naye.

Wakati mwingine unaweza kuwa unagombana na mpenzi wako kwa sababu tu, hamshabihiani kwa baadhi ya mambo ikiwemo kutokuridhishana.

Inawezekana wewe ni mwanamke ambaye unamuona mwanaume wako kama siyo mzuri kwa sababu hakuridhishi, vivyo hivyo mwanaume unaweza kuona mke uliyenaye siyo sahihi kwa sababu hujaridhika na jinsi alivyo.

Ukubali au ukatae, lakini ukweli ni kwamba, hakuna mwanamke mbaya, wanawake wote wako sawa isipokuwa inategemea na nini ambacho mwanaume amekipenda na kukielewa zaidi kutoka kwa mwanamke.

Ukitaka kuamini hilo, kuna mwanaume mwingine anaonekana ni mtanashati, lakini mpenzi au mke wake ni mwenye muonekano wa kawaida tu. Lakini ukweli ni kwamba mwanaume huyo inawezekana ameridhika na hali aliyonayo mwenza wake.

Ninachotaka kusisitiza ni kwamba kabla hujamhukumu mwenzako kwamba ni mbaya, ujiangalie pia mtazamo wako kwa huyo mwenzako. Huenda tatizo liko kwako pia na wala sio huyo unayedhani ana tatizo.

sizarinah@gmail.com 

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Usijitie zuzu, tia bidii kujua...

Mikopo: Wakenya wamchangia mwanaharakati