Makala

UMBEA: Iweje umeolewa na bado u mgeni wa kudumu kwenu?

April 19th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

TABIA zenu baadhi ya akina dada ambao aidha mmeolewa ama mnaishi na wenzenu, huwa zinatia kichefuchefu.

Unapoolewa, maana yake ni kwamba unaachana na wazazi wako na kuanza maisha mapya na huyo mwenzako.

Hata hivyo, hatua hii imekuwa ni changamoto kwa baadhi ya akina dada.

Kwani baadhi yao, hushindwa kabisa kujipa nafasi kutoka kwa wazazi wao na kujikuta kutwa wanashinda huko kwa wazazi wao.

Iwapo umeolewa na kila mwezi unaenda nyumbani kwenu kumsalimia mama yako, haumwi wala hana tatizo, lakini unaenda kumsalimia, yaani mbali na kuongea naye kwenye simu lakini bado huridhiki kila mwezi mara moja mbili unamuaga mume wako na kumuambia “naenda kumsalimia mama.”

Haiishii hapo tu, hata kwa ndugu zako wengine umekuwa ni mgeni wao wa kudumu, kila wakati unaenda kuwasalimia, hapo uelewe kwamba kuna tatizo na iwapo unaenda mfululizo kwa mama ama ndugu zako na hawajakueleza kwamba hiyo tabia yako haijakaa sawa, ni wazi kwamba kuna tatizo baina yenu wote.

Inawezekana hivi sasa unaona kawaida, kwa kuwa mumeo halalamiki, ama hajawahi kusema anakerwa ama kukwazika na tabia na mwenendo wako.

Uvumilivu hufika kikomo, lakini ipo siku atasema, ipo siku atachoka hiyo tabia yako atakuambia na kwakuwa wewe umeshazoea basi utaona ni kitu cha kawaida kwako, ama pia unaweza kumuona mume wako kama anawachukia ndugu zako ndiyo maana hapendi uende kuwasalimia.

Tena unaweza kujibu: “Mbona wewe kila siku unaenda kwenu kusalimia.”

Inawezekana hadi hapa umejitoa ufahamu na kujidai huelewi kinachozungumzwa ama labda kuona kwamba naingilia anga zako binafsi.

Iwapo hii ndiyo tabia yako, kwamba kwenu isipite sherehe umeshaenda, usitokee msiba huko kwenu hata kama ni wa mtu ambaye aliwahi kupita kwenu kuomba maji unataka kwenda ili mradi umetokea kwenu, kila mchango wa sherehe kwenu unataka kutoa basi kama mume wako hatakuchoka akakukataza basi ipo siku atakuacha kimya kimya, bila taarifa au hata akibaki nawe hatakushirikisha katika mambo yake ya maendeleo kwa sababu anajua akili, hisia na mawazo yako yote yako kwenu na wala sio pale ulipo na mumeo.

Hakuna ubaya kwenda kwenu kusalimia, si vibaya kuongea kila kitu na mama yako lakini ni muhimu kuwe na mipaka.

Kwanza katika mambo ambayo unamuambia mama yako, kwamba si kila kitu ambacho kinatokea katika ndoa yako ni lazima umuambie mama yako hata kama ni kwa wema, inafaa ujue mipaka inaanzia na kuishia wapi na wakati gani wa kuzungumza na wakati gani wa kunyamaza.

Lakini pia ni katika kumuambia mume wako, kwamba si kila siku ukiongea na mama yako nilazima umuambie mume wako, mara mama kakusalimia, mama kasema hivi, mama vile, mama anataka hiki, mama hataki hiki, jifunze kuweka breki kwenye mdomo wako.

Unapokua unamuambia kila kitu mume wako anaona kuwa unamsikiliza zaidi mama yako kuliko yeye anaona kuwa huna maamuzi binafsi, ama maamuzi yenu wawili kama wanandoa, bali unamtegemea mama yako katika kuwaza na unapokuwa unaenda au kuongea na mama yako kila mara mume wako hujua kuwa hakuna kitu mnaongea zaidi ya mambo ya familia yenu, unagawa siri za familia hivyo hakuamini tena kukuambia kitu akijua kuwa utamuambia mama yako.

Kila jambo lina mipaka yake, na lolote linalozidi huleta athari. Mtembelee mama yako, zungumza naye, lakini tambua mipaka yenu.
Badilika rafiki yangu.

[email protected]