Makala

UMBEA: Kabla kuhukumu keti chini utathmini kwa nini alionja nje

May 24th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

UTAPELI, hadaa ama figisu hutokea katika ndoa, mapenzi ama uhusiano wowote.

Kwamba mumeo ama mkeo anaweza kuonja nje ya ndoa, kujiliwaza ama sababu kuna yale anayokosa katika ndoa yenu.

Wakati mwingine jambo hili linapotokea huwa kuna sababu ya msingi kabisa. Yaani kuna sababu iliyomfanya mke ama mume aende nje.

Hata hivyo, yanapotokea haya, wengi humlaumu mhusika na kumhukumu kuwa hafai kabisa. Wachache sana hutuliza akili na kujiuliza sababu ya mmoja kwenda nje ya ndoa.

Ieleweke kwamba sichochei wala siungi mkono mwanamke ama mwanaume kutafunwa ama kutafuna nje ya ndoa. Lakini mara nyingi kama jambo hili linatokea mara ya kwanza, badala ya kumkashifu na kumlaani mhusika, ni vyema kwanza kujua sababu iliyopelekea yote hayo yafanyike.

Na kuna kaka zangu na dada zangu ambao hurukwa na akili kwa muda anapogundua mwenziwe ameperembwa nje. Na hatua wanazochukua wakati mwingine huleta madhara zaidi kuliko suluhu.

Baadhi yao huamua kwenda kuwaadhibu wale waliohusika na tukio zima, yaani yule mwanamke ama mwanaume aliyeonjwa ama kuonjeshwa nje ya ndoa. Kufanya hivi ni kukosa busara kabisa.

Kwani aliyetenda hivyo ni mke ama mumeo na yule mwingine alifuatwa tu na kukubaliana naye. Hivyo kama ni adhabu muadhibu mkeo ama mumeo.

Natambua hili jambo huwa linauma sana na linafanya upoteze imani yote kwa mwenzio japokuwa unampenda.

Upendo hauna maana ikiwa hakuna uaminifu, kwamba huwezi kumpenda mwenzio kwa asilimia zote wakati huna imani naye tena kutokana na kosa alilofanya.

Najua kuna baadhi ya watu wanaamini kuwa wapo watu wameumbwa hivyo.

Kwamba hata umfanyie nini atatoka nje tu. Katika hali halisi, binadamu akiridhishwa kabisa sio rahisi kwenda kutafuta kuburudishwa zaidi nje.

Udanganyifu katika ndoa hufanyika pia kwa sababu zingine mbalimbali.

Kuna wale wanaofanya hivyo ili kuwa na mpenzi wa pili wa kudumu.

Kuna wale wanaofanya hivyo ili kujaribu kupata mambo fulani ambayo hawayapati kwa wapenzi wao na hii huwa kwa muda mrefu.

Na kuna wale wanaofanya hivyo kwa bahati mbaya kwa vile kalewa, kashindwa kujizuia baada yakushawishiwa au alikuwa amekanganyikiwa kutokana na tatizo zito lililompata ghafla.

Ni wazi kuwa hili linapotokea uamuzi wa kwanza kabisa na haraka ni kuachana na mke, mume ama mpenzi wako.

Lakini je, unaweza kuendelea kuishi na mwenzio? Je, utaweza kumuamini tena? Utaanzaje kufanya naye mapenzi? Mambo yatakuwa kama zamani, ama kila kitu kitabadilika baada ya kugundua alionjwa na mtu mwingine?

Mapenzi ya dhati

Kakangu na hata dadangu, mwenzio anapokiri kwamba ameonjwa ama kuonja nje ya ndoa, mara nyingi anakuwa na mapenzi ya dhati kwako.

Anajutia kosa lake na pia anaumia kama unavyoumia wewe, ama pengine zaidi kwa kile alichokifanya. Na mwenzio anapotubu mbele yako, hata kabla hujamgundua, basi uwezekano wa yeye kurudia kosa ni mdogo sana.

Hii ni kwa sababu hapendi na hataki kuumia na kukuumiza tena.

Lakini yule anayeficha mpaka unagundua baadaye, ikiwa imepita miezi ama miaka kadha, hana tofauti kubwa na muuaji. Na ni wazi kwamba hana mapenzi ya dhati nawe.

Ukweli ni kwamba uchungu huwa ni ule ule mwenzio akikuambia kabla hujagundua, ama ugundue baadaye.

Lakini kama kweli mnapendana, hakuna kosa lisilosameheka. Ingawa itachukua muda mrefu kusamehe, lakini mnaweza kuanza kujenga upya uhusiano wenu.

Na wakati mwingine inabidi uanze upya kumpenda mwenzako na kujaribu kujenga imani naye. Hatua hii sio ndogo na inachukua muda mrefu. Inaweza kuchukua miezi na hata miaka.

Hivyo kabla ya kuhukumu, keti chini na tathmini, kwa nini mwenzio alionjwa nje.

[email protected]