UMBEA: Kile ambacho ni chako, utakipata tu hata kama kipo chini ya mlima

UMBEA: Kile ambacho ni chako, utakipata tu hata kama kipo chini ya mlima

Na SIZARINA HAMISI

MAISHA yetu huambatana na mizigo mingi tunayoibeba kiakili, kimwili na kiroho.

Katika maisha ya kila siku ni kawaida kuambatanisha na ndugu, watoto, wazazi na masuala mengine yanayotuhusu. Tunapokosa mbinu na ujuzi wa kutofautisha na kuachana na mizigo mingine tunayobeba kila siku, inakuwa rahisi kupata msongo wa mawazo na wakati mwingine kukosa amani na kujiona una majukumu ambayo yanakuendesha mbio.

Kuachana na mizigo hii mara nyingi sio rahisi, hasa inapobidi uachane ama utue kitu ama jambo ambalo unalitaka ama kuhitaji. Inaweza kuwa ni mtu ambaye unampenda ama jambo ambalo ni muhimu sana kwako. Kiuhalisia sio rahisi kutua moja kwa moja mambo ambayo tunayapenda lakini inabidi kufanya hivyo. Kuna njia na mbinu za kutua mambo mengi katika maisha yetu bila ya kuumia kupitiliza.

Mara nyingi tunaposhikilia watu ama vitu ambavyo vinatuumiza, huwa tunakuwa na matumaini kwamba hali itabadilika. Ingawa mara nyingi mtizamo huu huwa sio sahihi, kwani unaweza kupata uhusiano mwingine, unaweza kupata marafiki wengine, unaweza kupata jambo lingine pale unapotua yale yasiyofaa.Kuna usemi kwamba kile ambacho inabidi kiwe chako, utakipata hata kama kipo chini ya mlima. Na kile ambacho sio riziki hautakipata, hata iwapo kipo katikati ya vidole vyako viwili.

Katika maisha yoyote, jambo ambalo linakuwa gumu kuliko kawaida, ama linakusababishia maumivu na kukukosesha amani, hilo sio riziki yako. Kuwa na mtizamo kama huu katika maisha yetu ya kila siku, kunaweza kukupunguzia maumivu ya moyoni ama kukurahisishia kuchukua uamuzi wa kutua jambo linalokusumbua ama kuendelea nalo. Vitu ama mambo ambayo inabidi yawepo katika maisha yako, yatatiririka kwako bila kutumia nguvu na akili nyingi. Jinsi ambavyo unapambana kupata ama kutunza kitu ama jambo ambalo sio riziki yako, ndivyo nalo litakakavyopambana nawe ili liondoke katika himaya yako.

Kuachana na jambo ama kitu unachokipenda, ni jambo linalohitaji msuli wa moyo kwani ni vigumu. Wakati mwingine unaweza kuona kwamba haiwezekani kusonga mbele, kuachana na jambo ama vitu ambavyo vimekuwa na maana kwako. Ni vyema ukose utulivu huu wa moyo kwa muda kuliko kuishi katika hali ambayo itakuletea changamoto. Ukiachia jambo lisilofaa, unaokoa mengi katika maisha yako kwani ukiendelea kushikilia, athari yake huwa ni kubwa.

Wakati mwingine tunashikilia uhusiano usiofaa ama kuendelea kuwa na marafiki ambao hawafai tukihofia jinsi tutakavyojihisi iwapo tutavunja ama kutua watu hao. Lakini mara nyingi kuendelea kuwa katika hali hii huleta madhara zaidi ya faida. Kuna nguvu kubwa katika kutua uhusiano, mambo na vitu ambavyo vinatukosesha amani, nguvu ambayo hurudisha amani na utulivu katika maisha ya kila siku.

Pale unapopata ujasiri wa kutua mambo, vitu na watu ambao wanakuletea changamoto katika maisha yako, ndipo utakapotambua kwamba unapata nguvu mpya na nafasi ya kubeba yale yanayokufaa. Utatambua una nafasi ya vipaji vipya, kazi mpya, uhusiano mpya na vitu vingine ambayo vina umuhimu kwako.

sizarinah@gmail.com

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Ukipenda ama kupendwa jamani sichezee...

Tangatanga washabikia ‘uhasla’ wa Rais Biden