UMBEA: Kukutana na mtu mnayeendana ni kibarua ila usivumilie mateso!

UMBEA: Kukutana na mtu mnayeendana ni kibarua ila usivumilie mateso!

Na SIZARINA HAMISI

TUMEZOEA kusikia waliopo katika uhusiano ama ndoa wakiambiwa wavumilie.

Hata pale mwanandoa anapoelezea malalamiko yake ama kutofurahishwa na mwenendo wa mwenzake, sio ajabu akaambiwa avumilie kwani hivyo ndivyo ndoa ama uhusiano ulivyo.

Neno uvumilivu lisitumike vibaya kiasi cha kuharibu mfumo wako wa maisha. Kuna mengine hayavumiliki zaidi ya mara moja. Kuna tabia zenye kuumiza na kukera unapovumilia inakuwa sawa na kulea ugonjwa kwa kuufunika ukidhani utapona wenyewe baada ya muda.

Hivyo unapokuwa katika uhusiano ni vyema utathmini yale ambayo yanavumilika na yale ambayo kuyavumilia ni kujiletea shida. Iwapo unaona mpenzi, mume, mke au rafiki yako havumiliki kwa tabia zake, usihofie kukaa mbali naye. Usijipe nafasi ya kuvumilia kunyanyaswa, kupigwa ama kutukanwa hadharani hata faraghani. Pia usibebe mzigo wa kusalitiwa mara kwa mara ukidhani kwamba mwenzako atajirekebisha baada ya kukueleza kauli hiyo mara kadha.

Usijipe nafasi ya kuvumilia mtu asiyekuheshimu wala kukusikiliza hata mambo ya msingi. Kumbuka, siku zote anayependa na kujali sana katika mahusiano ndiye anayeishia kuumia. Wanasema mwenye upendo wa dhati hana bahati, kwani unaweza ukampenda sana mtu na akajua ila atapuuza hisia zako na kwenda kwa mwingine au kukusumbua makusudi akiamini kuwa huwezi kumuacha.

Pale mwenzako anapotaka kuachana nawe, kamwe usimlazimishe abaki kwako. Inawezekana bado unamhitaji ila yeye ameamua kuachana nawe. Huenda ameona amempata mwingine bora zaidi yako au amechoshwa na tabia zako. Ni afadhali muache aende, kwani huwezi kuzuia mafuriko. Japo ni kweli inauma kuachwa na unayempenda lakini yapokee maumivu ili yatakapoisha uendelee kuishi maisha yako. Ukilazimisha abaki kwako wakati yeye anataka kuondoka, atakuumia zaidi badala ya kukupa utulivu wa moyo.

Wapo wale wanaoamua kuvumilia kila aina ya udhalimu wakidhani kwamba pesa ama maisha mazuri waliyokuta hapo walipoenda yatawaletea amani na furaha. Siku zote pesa sio suluhisho la shida zote. Usjililazimishe kuishi kwa mtu ambaye anaonyesha bayana kwamba hana mapenzi nawe sababu tu ana uwezo mkubwa kiuchumi.

Ukweli ni kwamba huyo unayeamua kumvumilia kwa sababu hizo, hakuzaliwa peke yake duniani, na haileti maana kumng’ang’ania wakati anaonyesha matendo ama maneno ya kutokuheshimu au kukupenda. Na hata pale unapoamua kusonga mbele, usihofie kupenda tena baada ya kutendewa vibaya, kwani pia watu hawalingani. Na tabia na vitendo vya watu hutofautiana. Na sio wanaume wote “mzazi wao ni mmoja”.

Mapenzi mazuri ni yale yanayowakutanisha wapendanao ambao wanaelewana, wanasikilizana na kufurahia wakati mzuri. Pia wanakuwa pamoja wakati wa huzuni na majonzi. Hata hivyo, kukutana na mtu mnayeendana na kuelewana ni mtihani kidogo. Wapo wanaosukumwa na matamanio ya kimwili pekee. Katika yote, siku zote ielewe thamani yako, thamani ya uhusiano uliopo na thamani ya utu wako. Unapoona kwamba mwenzako hatilii maanani yale ambayo ni ya msingi kwako na anakuonyesha wazi kwamba hauna kipaumbele kwake, hautajitendea haki kuendelea kuishi katika mazingira ya aina hiyo.

sizarinah@gmail.com

You can share this post!

Hofu ugonjwa wa kutatanisha ukienea Nakuru

FATAKI: Ikiwa wewe bahili wa mali na moyo, basi mapenzi...