Makala

UMBEA: Kumjali ni sehemu kubwa katika suala la mahusiano

January 31st, 2020 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

UNAPOPENDWA, ukapendeka na upende ukapendwa, furaha, utulivu na amani huwa ni rafiki zako wa karibu.

Wataalam wa masuala ya mahusiano wanasema katika upendo huu, mwanamke ndiye ana uwezo zaidi wa kupenda kuliko mwanaume. Kwamba mwanamke akipenda, anapenda hadi anazubaa.

Kwa upande wa mwanaume, huwa wanapenda kwa hesabu, ni nadra kupata mwanaume kazama kwenye mapenzi kiasi kwamba anazubaa na kuduwaa.

Wengi huwa wanatanguliza majukumu na ndio maana sio vigumu kwa akina kaka kuwa na mwanamke zaidi ya mmoja na akaweza kuwamudu wote kwa pamoja.

Ni tofauti kidogo kwa mwanamke. Kwani ni wachache sana waliojaliwa kipaji cha kuwa na wanaume wengi kwa wakati mmoja na kuweza kuwaridhisha wote kwa pamoja.

Na ndiyo maana sio vigumu sana kugundua mwanamke anapoanza usaliti, kwani uwezo wa hadaa ya mapenzi sio mkubwa kiasi cha kuficha hisia walizo nazo.

Mwanamke akifanya mapenzi na akaridhika vizuri, ana uwezo wa kuonyesha upendo na asitamani mwanaume mwingine hadi pale atakapoona upendo na mapenzi yanapungua.

Mwanaume ana hitaji zaidi ya heshima na utii kutoka kwa mwanamke na sio tu kurushwa roho kutamfanya asisaliti. Lakini wanawake walio wengi huganda katika mahusiano kwa sababu ya kuridhika na tendo la ndoa zaidi ya vitu vingine.

Mwanamke akifanya mapenzi akaridhika, ana uwezo wa kukaa bila tamaa ya kufanya tendo la ndoa hata zaidi ya miezi minne ikiwa yuko mbali na kishawishi au mpenzi wake. Lakini mwanaume ana uwezo wa kufanya mapenzi hata zaidi ya mara tano kwa siku na mwanamke mmoja au wanawake tofauti.

Mwanaume ana uwezo wa kumaliza kufanya tendo la ndoa na kupoteza hisia kwa kiwango kikubwa sana kuliko mwanamke ambaye ubongo wake una uwezo wa kutunza kila aina ya hatua katika tendo la ndoa.

Hivyo hali halisi ni kwamba mwanaume hatekwi na mapenzi kwa sababu ya kurushwa roho mfululizo, bali hufurahia zaidi kuheshimiwa na kutambuliwa jukumu lake la kutimiza mahitaji ya mwenzake ama familia.

Baadhi ya akina kaka wanadhani kumwambia kuwa mwanamke unampenda kunamaliza kila kitu katika mahusiano, bila kujua kuwa unapoamua kumshirikisha katika maisha yako kunamfanya akuamini na akupende zaidi.

Masuala ya pesa yanachukua nafasi kubwa. Kwa mwanamke anayekupenda na anataka kufika mbali nawe, kawaida anakuwa mwoga kukuomba hela, hata kama yuko na shida hawezi kuwa mwepesi wa kutaja kuwa anataka hela, na hata kama anataka hawezi kusema kiwango cha juu kama ambavyo ingekuwa kwa mwanamke ambaye yuko na mwanaume kwa sababu ya maslahi binafsi.

Pia uelewe kwamba baadhi ya wanawake wana tabia ya kukaa kimya hasa pale ambapo wanakuwa hawajafikishwa wanapotaka wanapokuwa faragha. Inaweza kuchukua hata mwaka na bado akashindwa kabisa kukukosoa kuhusu hilo, hivyo muda mwingine inabidi uwe mbunifu kujua na kumuuliza maswali ambayo yatamfanya naye afunguke kile kilichopo moyoni mwake. Ni kweli wanawake ni wavumilivu lakini wanaweza kuchoka kuvumilia hilo na wakajikuta wanajaribu na nje pia.

Mwanamke anapenda kuonyeshwa kwamba ni wa muhimu kwa mwenzake, kumuonyesha kwamba unamjali. Mwanamke anapenda asikilizwe, uwe karibu naye, anapotaka kitu umsikilize na hata kama unataka kukataa, basi umpe neno la maana jepesi la kumjibu ili kuridhika na uhakikishe kuwa ameridhika.

Wakati mwingine mdekeze, mbembeleze. Ni mambo madogo, lakini yanayoleta tofauti kubwa katika kuhusiana na mwanamke.

 

[email protected]