Makala

UMBEA: Kumpenda mtu kwa dhati kunahitaji mbinu na mikakati

March 28th, 2020 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

KATIKA kipindi hiki ambacho kuna sintofahamu, kutiliana shaka na hata kutengana, ni muhimu kujenga hulka ya kujaliana pia.

Iwapo umewahi kupenda ama unapendana na mchumba, mpenzi ama mume wako na mko katika uhusiano wa kimapenzi, jambo kubwa linaloweza kuwaunganisha ni upendo.

Unapopenda kwa dhati, tegemeo kubwa ni kwamba mwenzako pia akupende kwa vitendo na sio maneno matupu. Je, ni wangapi wamefanikiwa kuwafanya wenzao wawapende zaidi namna wanavyotaka wao?

Kati ya wengi walio katika uhusiano ni wachache sana wamefanikiwa kufaulu mtihani huu. Wengi wao wanalalamika kuwa wenzao hawawapendi kwa kiwango wanachotamani kupendwa. Ni vyema ikatambulika kuwa japo mapenzi huchukuliwa kama jambo la kawaida, kumpenda mtu mwingine kwa dhati huhitaji mbinu na mikakati.

Ukweli ni kwamba hakuna mwanamke au mwanaume anayeweza kumpenda mtu kisirani, mlalamishi na asiyependa masikilizano.

Hata kama mhusika alimuona mwenzake na kumpenda, iwapo atakuwa na tabia tata na hataki kubadilika, upendo wa mhusika utashuka na kama itawezekana anaweza kuanzisha mahusiano na mtu mwingine.

Ni nani atampenda mwanamume mvivu, asiyejituma na mwenye kupenda zaidi starehe na watu wengine huku akimsahau yeye? Hata kama mwanamume husika anampenda sana mwanamke huyu ila kama matendo haya ya ovyo hayatokoma, basi mwanaume huyu anaweza kuangalia ustaraabu sehemu nyingine.

Kuna mbinu za kumfanya mwandani wako azidi kukupenda na kukujali. Azidi kukuona wa thamani na wa maana katika maisha yako.

Baadhi ya akina dada hudhani urembo pekee unatosha kuwafanya wapenzi wao wazidi kuwapenda na kuwajali. Lakini uzuri wa mwanamke sio sura pekee. Mwenendo na vitendo ndivyo huangaliwa kwa kiasi kikubwa.

Hakuna mwanamume ambaye atafurahia kuwa na mwanamke kiburi na asiyeonyesha kumjali wala kumthamini. Ni kiu ya kila mwanaume kuwa mfalme kwa mke wake. Yaani awe na kauli juu yake, awe na uwezo wa kutoa maelekezo na yakatekelezwa, awe na mwanamke mwenye kumtendea vile anavyotaka yeye.

Ni maajabu pekee ndiyo yanaweza kunusuru penzi ambalo mwanamke anajiona kidume na mbabe dhidi ya mume wake.

Kwa upande wa pili mwanamke anahitaji kuwa na mwanamume ambaye atamfanya ajiamini na ajithamini. Sio mwanamume kila wakati ni kulalamika tu. Badala ya kutoa dukuduku lako, unakuwa ni mlalamikaji wa mfululizo. Badala ya kupambana na changamoto za maisha, kila wakati unakuwa na visingizio visivyoeleweka.

Mwanamke anataka kuwa na mtu ambaye atamfanya kuona changamoto zote wanazopitia ni kitu cha mpito. Unapokaa naye na kuanza kulalamika kuhusu hali ngumu badala ya kupambana bila kelele, unaweza ukamtisha na kumtia hofu ya furaha ya maisha yake akiwa nawe.

Mwanamke anahitaji kutulia akili, si kujazwa msongo wa mawazo. Hata kama familia mnapitia kipindi kigumu cha uchumi si jukumu lako mwanamume kila muda kukaa na kulalamikia hali hiyo. Pambana na hali yako, hata pindi mwanamke wako akianza kulalamikia hali ngumu, ni jukumu lako kumtia nguvu tena kwa sauti ya kujiamini.

Mwanamke anataka mwanamume wa aina hii, si mwanamume ambaye kila muda anasema; “Unajua mpenzi hali hii ni ngumu sana sijui huko mbele itakuaje?” Kisaikolojia ukiwa mtu wa hivi mwanamke wako ataanza kufikiri tofauti. Mwanamke sio mvumilivu mkubwa wa mikiki. Hao unawaona wako katika mikiki, wako kwenye hali hiyo sababu ya mazingira magumu.

Ili kudumisha amani na furaha katika mahusiano yako, mwanamke jitolee kwa kiwango kikubwa kwa mume wako ili naye ajione yuko na mtu sahihi katika maisha yake. Furaha na amani itawale kipindi hiki kwa wote

 

[email protected]