Makala

UMBEA: Lugha kavu, tena ya mkato ni dalili mapenzi yaanza kuchuja

October 5th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

HAYA maisha tunaishi hapa duniani sio ya kudumu.

Yana mwisho wake.

Hivyo usimtese, kumkwaza ama kumkomesha mwenzako.

Utambue kwamba una kipindi tu cha kuwepo na kipindi hicho kikifika, utazikwa na kufukiwa kama gunia la maharagwe.

Mwenzako anapokutafuta kwenye simu, halafu unampuuza ama hata kumkatia simu huku ukitabasamu, jiulize iwapo vitendo hivyo vya kikatili utadumu navyo milele.

Pale unapotoa kisingizio kwamba una kazi nyingi, huna nafasi ya kuwasiliana ama hata kumuona mwenzako bila kujua kwamba unaumiza moyo wake, jiulize iwapo utaishi milele.

Iwapo umemchoka, ama humtaki tena mwenzako, mweleze ili aendelee na maisha yake kwani pale unaposema wa nini, wapo wengine huko nje wanaojiuliza watampata lini.

Hangaiko la mwenzako kukutafuta ikiwemo kukuona uso kwa uso au kukusikia kwa njia ya simu kwa siku linakuwa ni kibarua kisichokuwa na ujira kwake, uelewe kwamba moyo sio mwanasesere, kwamba utauchezea uupige dana dana na kuurusha huku na kule.

Upendo ni hisia na hisia hazionekani kwa macho, zinaonekana kwa vitendo na njia kuu ya upendo ni mawasiliano.

Mahusiano hayakui kwa kusema tu nakupenda, mahusiano hayaimariki kwa zawadi bali yanakua na yanaimarika kwa ninyi kuwasiliana mara kwa mara.

Unaweza kutambua kwamba mahaba yamejaa moyoni mwa mwenzako pale anapokutafuta kwa bidii unapopita muda fulani bila kuwasiliana nawe. Ama pia nawe unapohisi hali hiyo ya moyo kukosa utulivu unapokosa kuwasiliana na mwenzako kwa muda fulani. Utajihisi mpweke na ukihangaika moyoni pale unapokosana naye kwa muda.

Iwapo upo kwenye mahusiano hai, yasiyokuwa na migogoro mfululizo, basi pia mawasiliano yenu yatakuwa ni mazuri na yenye afya tele.

Wapo wale wataalamu kwa kudai wametingwa na kazi hawana muda hata wa kujibu ujumbe mfupi ama hata kupiga simu ya kutaka kujua mwenzake anaendeleaje.

Wakati unapomwambia mwenzako umetingwa na kazi, shughuli, biashara, kwanza jiulize katika huko kutingwa kwako unashindwa kutumia sekunde mbili za kumtaarifu mwenzako kinachoendelea?

Kabla ya kuanza mahusiano lazima ujue mahusiano ni gharama, iwapo hutaweza kugharimika kulinda mahusiano, kujenga mahusiano, basi usiingie kwenye mahusiano, utamsumbua bure mwenzako na kumpotezea muda wake.

Ukiona mwenzako katika mahusiano ana mazoea ya kukwambia ametingwa na kazi na kwamba hana nafasi, basi ni bayana umeanza kuchuja moyoni mwake na umuhimu na uzito wako kwake umepungua.

Jiandae kisaikolojia tamati inakaribia. Huenda kuna mtu anajaza ama ameshajaza nafasi yako na ukikosea kidogo tu, unalimwa buti na kujikuta nje ya uhusiano, kwa maana nyingine umeachwa.

Unapoona pia mwenzako hana tena mazungumzo nawe, mnapokutana ni salamu na kisha kila mmoja anashughulika na simu yake, hakuna majadiliano, hakuna mazungumzo, ni wazi kwamba shimo la kufukia uhusiano wenu limeshachimbwa linangoja mmoja wenu atumbukie lifunikwe.

Mlioko kwenye mahusiano yoyote, kwa nini umtese mwenzako kama huna mpango naye? Tena kwa nini usimwache huru? Kwa nini uendelee kumpotezea muda kukutafuta huku unamwambia huna nafasi ukijua bayana ameshatoka moyoni mwako?

Mawasiliano mliokuwa nayo mwanzoni yalikuwa moto, kuonana kwenu ilikuwa kila wakati, kupigiana simu yalikuwa maisha yenu, utani wa hapa na pale ni jambo la kawaida.

Ukiona sasa zinapita siku tatu hadi wiki hamjaongea wala kuonana. Na mkiongea ni dakika mbili na lugha unaisikia siyo ya mapenzi ya dhati. Inakuwa lugha kavu kavu, majibu ya mkato na wakati mwingine majibu ya kukwaza, hapa ndipo uanze kuandaa moyo wako, kwani dalili zote za kujeruhiwa hisia zinakuwa zinakunyemelea.

 

[email protected]