Makala

UMBEA: Maisha ya ndoa yapo katika hatua 3: Raha, ujana na uzee

October 11th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

MAISHA ya ndoa siku hizi yamekuwa kitendawili kwa wengi.

Mapenzi ndani ya ndoa nyingi siku hizi yamepungua na kwa wengine hayapo kabisa.

Wengi wanapoingia kwenye ndoa hutegemea zaidi mazuri bila ya kuweka nafasi ya changamoto zinazoweza kujitokeza.

Maisha ya ndoa yamegawanyika katika hatua kubwa tatu, ambazo kama utazielewa na kuzitafakari kabla ya ndoa, kuna uwezekano wa kupunguza changamoto zinazoambatana na maisha hayo.

Ndoa huwa tamu sana katika mwaka wa kwanza wa kuishi pamoja, wengine huita kipindi hiki mwaka wa asali, kipindi cha raha, utulivu, mapenzi, maelewano baina ya wanandoa. Si lazima kiwe mwezi mmoja kama watu wengi wanavyoamini, bali kinaweza kikawa chini ya mwezi mmoja au zaidi ya mwezi mmoja.

Wengine kipindi hiki huwa kifupi sana, wapo ambao kinadumu kwa mwaka mmoja, lakini pia wapo ambao wanakishuhudia kwa mwezi, mmoja ama miwili na hali inaanza kubadilika. Iwapo mtafanikiwa kupita salama kipindi hiki, awamu inayofuatia, naiita ujana wa ndoa. Muda huu wanandoa wanakuwa wameshatambuana tabia na kuelewa mtizamo wa mwenzake kwa mambo mengi, mwelekeo wake na matarajio yake.

Hapa ndipo ndoa nyingi hujengeka au kuvunjika. Kwani katika muda huu kila mmoja anaishi maisha ya uhalisia na wala sio yale ya kufikirika.

Iwapo wote wawili wana nia ya kuwa pamoja, kipindi hiki ndicho ambacho kinatakiwa uvumilivu mkubwa wa kuelewa tabia na mwenendo wa mwenzako. Muda unaotakiwa urekebishe yale yanayomkera mwenzako, au ukubali udhaifu unaomhusu mwenzako.

Ni muda ambao watoto wanazaliwa na majukumu yanaongezeka. Wakati ambao wote wawili mnatakiwa mjue jinsi ya kupalilia penzi na jinsi ya kuweka muda wa kuwa pamoja mara kwa mara.

Kipindi hiki ni kipindi ambacho wanandoa wanakuwa tayari wameishaingia katika majukumu ya kulea kwa kupata matunda ya ndoa yao ambayo ni mtoto au watoto.

Hapa pia wapo wanaokwama, kwani ndicho kipindi kigumu zaidi kwenye ndoa. Kama muda huu utapita na kuwaacha mkiwa salama, hatua inayofuata ni uzee wa ndoa.

Hapa ndipo kunakuwa na kuchokana kwa wanandoa, kusababisha migogoro mingi na hata kufikia familia kuvunjika au kuishi kwa ajili tu ya kulea watoto na si vinginevyo.

Hapa ndipo unakuta wanandoa wanaishi pamoja na kwa nje wengi wanadhani ni mke na mume wanaopendana, lakini ukweli ni kwamba wanaishi pamoja kama ndugu, huku kila mmoja akiwa na maisha yake ndani ya nyumba moja.

Wengi wao wanaishi sababu ya watoto ama pia kwa kujali matarajio na kauli za jamii zao kuhusiana na ndoa.

Hali hii huitwa talaka ya kimapenzi, talaka ya uhusiano na mara nyingi hufuatiwa na michepuko mfululizo kwa mume na wakati mwingine hadi mke katika harakati za kuziba pengo wanalolikosa kwenye ndoa.

Kabla ndoa haijafikia kuzeeka, kuna visababishi vinavyopelekea kuzeeka kwa ndoa au kuchokana. Visababishi hivi ni vitu ambavyo hupuuzwa hususan na wanawake na kuonekana ni vitu vidogo, kumbe ni vitu vikubwa mno.

Kwa upande wa mwanamke, ni kutojali usafi wa mwili na hata makazi, mavazi anayovaa, chakula anachopika, nidhamu ya nyumba na mpangilio kwa ujumla. Upande wa mwanaume, kutokidhi majukumu yake ya familia, kutomjali mkewe na kumuonyesha mapenzi kwa vitendo na kumtoa kasoro kwa vitu ambavyo anaweza kumezea ama kuvipuuza. Pia kutomsikiliza pale anapokuwa anahitaji kutoa ya moyoni.

Katika yote ni muhimu kuelewa hatua iliyopo katika ndoa yenu na jinsi mnavyoweza kuepuka ibilisi wa talaka.

 

[email protected]