Makala

UMBEA: Mapenzi yapo tuyafurahie si kutuendesha kama gari bovu

August 17th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

WAPO watu ambao ni ving’ang’anizi wa mapenzi.

Kwamba yupo na mwenzake, anapigwa matukio tata mfululizo, lakini bado anaamini kwamba anapendwa sababu yeye anampenda sana huyo mwenzake.

Hii huwa naita jehanamu ya mapenzi. Ukidhani kwamba umepata kumbe umepatikana.

Mapenzi huweza kumfanya mtu akaishi maisha ya raha hasa pale anapompata mtu mwenye penzi la kweli lakini pia usipoyajulia, mapenzi yanaweza kukutoa roho. Wangapi leo hii wamechanganyikiwa kutokana na kukataliwa penzi na watu waliotokea kuwapenda? Wangapi wamejiua baada ya kuachwa na wapenzi wao? Wangapi wanashindwa kufanya kazi zao kwa ufasaha kwa sababu wamekorofishana na wapenzi wao?

Sio ajabu hata wewe umeshawahi kujiuliza na mpaka sasa hujabaini ukweli wa penzi lake kwako na kama hujawahi kujiuliza swali hili, basi hauko makini katika uhusiano wako. Iwapo unajiamini kwamba umepata mtu ambaye anakupenda kwa dhati, una uhakika gani wa hiyo imani yako? Unajuaje kwamba hauzungukwi mbuyu na kuchezwa shere mchana kweupe.

Hali halisi ni kwamba, mapenzi ya sasa yamejaa ulaghai wa kupitiliza. Unaweza ukajikuta uko na mpenzi ambaye anaonyesha kukupenda sana kiasi cha kukufanya uamini kwamba umepata mtu sahihi lakini kumbe anajifanya tu, anacheza mchezo wa kuigiza mchana kweupe tena bila aibu.

Hivyo wakati mwingine inawezekana huyo uliye naye awe ni dada ama kaka anakupotezea muda wako. Hatua muafaka ya kuchukua ni kufanya tathmini na uchunguzi wa kina kubaini ukweli wa penzi lake kwako. Niseme tu kwamba, hakuna mtu anayeweza kuwa na uhakika wa asilimia mia moja kuwa mpenzi aliyenaye amepata mtu kwa maana ya mtu kwelikweli na kama unaamini hivyo, unaifurahisha tu nafsi yako kwa kuwa ukweli unaweza usiwe huo.

Moyo wa binadamu ni kichaka, hivyo huenda mwenzako ameweka siri moyoni mwake, na ndio maana unaweza kukuta mpenzi wako anakusisitizia kwamba anakupenda lakini bado unashindwa kuamini.

Wataalamu wa masuala ya mapenzi wanasema, kumdhihirishia mpenzi wako kwamba unampenda sio lazima uropoke kila wakati kwamba nakupenda kama mpiga tarumbeta. Vitendo vyako ndivyo vitamfanya aamini hivyo.

Hata hivyo, hukatazwi kumpenda mtu lakini inapotokea unampenda mtu asiyekupenda na ukalazimisha akupende ili kujiridhisha, hali huwa ni tete.

Wengi wako kwenye aina hii ya mapenzi.

Kwamba msichana anaona mwanamume ni kichefuchefu lakini anamng’ang’ania kwa sababu anampenda. Hivi mwanamke kama huyu anashindwa kubaini kuwa mwanaume aliyenaye hana penzi la dhati kwake.

Ifike wakati ukae chini na utafakari penzi analokupa mpenzi wako na kuchukua uamuzi sahihi, kumuacha au kuendelea naye.

Haipendezi kupotezewa wakati na mtu asiyelithamini penzi lako.

Ni wakati muafaka wa wewe kujiuliza kama umepata au umepatikana, na kama umepatikana, jinasue lakini kama umepata, basi tulia na uyafurahie maisha yako.

Walio katika aina hii ya mapenzi wako wengi. Mtu anaona kabisa mwanaume anamuonyesha dharau, hamjali lakini bado anamng’ang’ania tu eti kwa sababu anampenda. Huku ni kupenda ama ni aina mpya ya ugonjwa ulioingia moyoni mwako?

Wakati umefika dada, ama kaka utafakari na kulipima penzi analokupa mpenzi wako na kuchukua uamuzi sahihi. Inakuwaje unapotezewa muda na mtu asiyethamini penzi lako, anayekuona kama sanamu ya majaribio na wala sio mtu mwenye thamani kwake.

Mapenzi yameletwa duniani tuyafurahie na wala sio yatutese na kutuendesha kama magari mabovu.

Penzi la kweli hujidhihirisha na wala halilazimishwi.

 

[email protected]