Makala

UMBEA: Mwanamke unapaswa kuvaa uhusika wa kike, sio jike dume

November 7th, 2020 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA kuolewa ama kutoolewa ni majaliwa.

Lakini mara nyingi zipo sababu zinazochangia kwa akina dada kutangatanga bila kupata mwenzake wa kutulia naye katika ndoa, kwa wale wenye nia ya ndoa.

Na mara nyingi hali hii huchangiwa na mwenendo wa akina dada hawa ambao hufanya wanaume wawahofie, wawakimbie ama wawatumie na kuwatupa kule.

Ni vyema wakati wote kujitathimini kitabia ili utakapoona udhaifu wako, basi uufanyie kazi na uweze kupata mtu sahihi wa kukuoa.

Waswahili wanasema afya yako inatokana na jinsi unavyokula na kuishi. Wakati mwingine hata aina ya ugumu wa kutoolewa unaoupitia kwenye uhusiano unatokana na jinsi wewe mwenyewe ulivyojiweka.

Hali halisi ni kwamba baadhi ya wanawake wamekuwa wakipoteza sifa za kuolewa kwa kukosa haiba ya kike. Mwanamke unapaswa kuuvaa uhusika wa kike. Hii inawahusu akina dada wenye tabia za jike dume. Uwe mwanamke kwa jina na pia vitendo, hata pale mtu akikuona ama kukutana nawe anajua kweli amekutana na mwanamke.

Haiba ya mwanamke si kuwa mzungumzaji sana kwa mwanaume hususan mwanaume wake. Mwanamke mwenye haiba ya kike ana heshima, mpole, mcheshi na mkarimu. Anajua jinsi gani mume anapaswa kuheshimiwa. Anajua azungumze vipi na mwanaume. Azungumze nini na wakati gani. Hata kama ana hoja ya kuzungumza au kumkosoa mwanaume wake, hawezi kuzungumzia hapo. Atatafuta muda mzuri wa kuzungumza na mwanaume wake tena katika lugha rafiki.

Kuna baadhi ya wanawake wanakosa waume wanaowatarajia sababu ya jinsi wanavyojiweka. Hawauvai ule uhusika wa kuwa mtu ambaye anakwenda kuwa mke au mama wa familia. Mwanamke anayejiandaa kuwa mke wa mtu anajua kuzingatia majukumu yake. Sio mwanamke unavaa mavazi kama ndege aina ya mbayuwayu, unaishi maisha ya kihuni, mtaa mzima unajulikana wewe. Mwanamke anayejiandaa na maisha ya heshima ya kuwa mke, anavaa mavazi ya heshima na anajiheshimu kwa jinsi yoyote anayoijua.

Mwanamke mwenye haiba ya kuwa mke ni mvumilivu wa mambo. Ana staha katika kuzungumza jambo. Anatambua utu ni nini, shida na raha; si mtu wa kupenda tu maisha mazuri bali anatambua pia kuna nyakati za vipindi vigumu katika maisha. Anatimiza wajibu wake ipasavyo kwa kumtia nguvu mwenzake. Anakuwa na mtizamo kwamba iwapo wamekosa katika wakati uliopo, bila shaka kesho mambo yanarekebishwa.

Wanawake wengine hawaolewi sababu ya kuwa na gubu. Wanawake ambao wanapenda kukasirika ovyo, kupenda ugomvi kila wakati au kusababisha kelele za kila wakati. Kupata mwanaume anayeweza kuvumilia tabia hizo ni nadra sana.

Wanaishia kuhangaika muda mrefu maana akina kaka hawapendi kero ndani ya nyumba. Wanachoshwa na mambo mengi ya maisha, wanatamani zaidi kupata faraja kwa wenzao na si kuongezewa kelele na hekaheka.

Katika yote kumbuka kwamba tabia huumba mtu na mwelekeo na mtizamo wako unategemea zaidi tabia yako na unavyohusiana na wengine.

[email protected]