Makala

UMBEA: Ndoa haijengeki kwa usiku mmoja, yahitaji uvumilivu

June 15th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

NITAZUNGUMZIA maisha ya ndoa, hasa kwa wale walioko katika muunganiko huu kwa muda wa kuanzia miaka mitatu na kuendelea.

Kama tayari upo kwenye ndoa na umeweza kudumu na mwenzako katika muda huu wa kuanzia miaka mitatu na kuendelea, tafadhali jipongeze nami naongeza kwa kusema hongera.

Muhimu bila kujali imani yako, ndoa inahitaji kumtanguliza Mungu mbele, tena sana, kujiombea mwenyewe na kumwombea mume wako na watoto mliojaliwa ama ambao mnatarajia kujaliwa.

Unapoona watu wamedumu pamoja kwa muda, utambue kwamba ndoa haijengeki kwa usiku mmoja.

Kuweza kuishi na mwenzako, ambaye mmekutana mkiwa watu wazima na kila mmoja akitoka katika mazingira yake kunahitaji nidhamu, uvumilivu na moyo wa kutokata tamaa, mrejesho kwa mwenzako pale ambapo unaona mambo hayajakaa sawa na mnahitaji kuyanyoosha ama kukubaliana.

Inafaa pia ujue ndoa sio kiwanda cha majaribio, kusema kwamba utakaposhindwa kwa mwanaume mmoja, basi utajaribu hapa na pale kama karata za pata potea.

Wengine wanasema ndoa inaleta heshima, lakini heshima hiyo inafaa kubebwa na kuthaminiwa na wote wawili. Heshima huwa ni pande zote na sio upande mmoja.

Hivyo usitarajie uheshimiwe wakati unashindwa kumheshimu mwenzako.

Ndoa inaleta heshima lakini heshima hiyo lazima ibebwe na ithaminiwe na wote wawili.

Ukweli utasemwa, hadaa katika ndoa zipo kwa mume na mke.

Kuna aina nyingi za hadaa, kwani wapo akina dada ambao hadaa zao ni za kuonja onja, ama kudokoa dokoa kama ndege, kwamba pale wanapokabiliwa na changamoto nzito, wanawasiliana na wapenzi wao wa zamani kutafuta faraja ama hata kukumbushia yale yaliyowavuta pamoja.

Kukumbushana huku kunaweza kusiwe muingiliano wa kimwili, lakini kunahusisha maneno ya mahaba, ujumbe mfupi wa mahaba na hata mazungumzo marefu katika simu.

Akina dada hawa ni waoga kuweka utupu wao ovyo.

Hali kadhalika akina kaka nao huwa wana tabia hii ya hadaa, hata wakati mwingine hata wakiwa wanapata kila jambo kwa wake zao, bado watachepuka na mchepuko wao huenda zaidi ya maneno ya simu. Wengi hujichangamsha kwa mahaba haramu na hata kuvuna matunda wasiyopanda.

Iwapo kaka utaona kwamba inakubidi umhadae mwenzako, tenda hivyo kwa heshima na usiri, linda aibu yako na ya familia yako.

Wengi hapa watasema inakuwaje anihadae iwapo ananipenda, sijui eti akinihadaa naondoka zangu, utawaacha wangapi dada, labda ufunge ndoa na mwanaume suruali, yule asiyekuwa rijali.

Halafu kuna wale wanaume ambao wanahadaa wake zao na kujivinjari na wasichana umri wa mabinti zao, wakaingia gharama kuwatunza, wakati wanajua bayana uwezo wao kwenye burudani unatia mashaka.

Yaani safari moja tu anakuwa hoi, chali hawezi tena chochote.

Ingawa msichana uliyemuopoa atakusifu, tena akikipa heshima kitambi chako, kumbuka kuna wanaume rijali ambao shughuli zao ni nzito, anavuruga kuanzia chumbani, sebuleni, jikoni hadi msalani.

Pamoja na yote, kumbuka kwamba vitu hivi vipo.

Hata pale unapodhani mumeo ni malaika, asiyeweza kudhuru hata nzi, lakini ukweli ni kwamba huenda anatenda hayo kwa siri na tena akijaribu kutunza heshima yako na familia yako.

Wapenzi wa zamani

Kwa wanawake pia vitu hivi vipo, ingawa wengi watajidai wao ni safi wasiokuwa na doa lolote la hadaa, lakini wengi ni mahodari wa kuwasiliana na wapenzi wao wa zamani na wakati mwingine wakikesha kutumiana jumbe za mahaba.

Katika yote tunza siri ya ndoa yako, haifai kwenda kuropoka nje.

Yanayowezekana yasuluhishe na mwenzio, ikishindikana wahusishe watu ambao una uhakika watasaidia kuleta suluhu.

[email protected]