UMBEA: Si kila wivu ni mbaya, wakati mwingine hujenga uhusiano kudumu

UMBEA: Si kila wivu ni mbaya, wakati mwingine hujenga uhusiano kudumu

Na SIZARINA HAMISI

PALIPO na upendo wa dhati, wivu pia upo.

Na pale unapokosekana ni vigumu kupata wivu na mara nyingi hili ni thibitisho la mapema kwamba hakuna hisia baina ya wahusika.

Wivu ni maumivu au wasiwasi wa kihisia! Inawezekana mwanzoni, wivu kwako ulikuwa msamiati lakini baada ya kuanza uhusiano, ghafla unajikuta unazingwa na mateso ambayo hayaonekani. Yaani umemuona mpenzi wako anazungumza kwenye simu na hauelewi, hicho unachohisi moyoni ndiyo wivu.

Wivu ni nini hasa? Katika kamusi ya Kiswahili, wivu ni hali au tabia ya mtu kusononeka au kukasirika pale ambapo anamuona mpenzi au rafiki yake ana uhusiano wa kimapenzi na mtu mwingine. Hata hivyo, maana hii haitoshelezi.

Kuwa na kijicho au gere, uhasidi pia ni tafsiri nyingine za wivu. Hata hivyo, pamoja na upana wa neno lenyewe katika ulimwengu wa sasa, maana hizi bado hazitoshi kutoa maana inayokusudiwa. Wivu ni hisia zenye utandu wa hofu, zinazosababishwa na hali ya kudhani kuna ushindani wa kimaslahi katika suala zima la kimapenzi. Hisia hizo zinaweza kujumlisha na maumivu yanayotokana na wasiwasi wa kuhisi hakuna uaminifu kati yako na mwenzi wako. Kuna aina tatu za wivu;

•Wivu wa mashindano: Hii hutokea pale ambapo kuna hali ya kushindana. Yaani kuna mtu mwingine anakuwa na lengo na mwenzi wako, hivyo unajitahidi kumbakiza kwenye himaya yako. Ukimuona naye moyo wako hautakuwa sawa.

•Wivu wa kusingizia: Hii inamaana kuwa unakuwa unamtuhumu mpenzi wako kwamba ana wivu kupindukia, wakati ni wewe mwenyewe ndiye unayesumbuliwa na wivu.

•Wivu wa kujidanganya kimawazo: Hapa unakuwa hauna imani na mpenzi wako, kwa hivyo ukikaa unakuwa na fikra kwamba mwenzio anakusaliti au anafanya yasiyopendeza, wakati hilo halipo.

Je, wivu ni mbaya kila siku? Kwa kifupi ni kwamba si kila wivu ni mbaya. Wakati mwingine una faida zake na umewezesha uhusiano wa wengi kudumu. Kitaalamu, inashauriwa kwamba kiasi fulani cha wivu ni muhimu kwenye mapenzi. Sayansi ya saikolojia inatoa muongozo kuwa hisia zako za wivu zinaweza kukusaidia kukulinda kwenye uhusiano wako.

Faida za wivu ni kama vile kuongeza kiwango cha mawasiliano. Mpenzi wako akiwa anakuonea wivu, atakuwa anakupigia simu mara kwa mara, hivyo kusaidia kuwaweka karibu.

Wivu husaidia kutoa tafsiri ya mipaka kwenye uhusiano, mko pamoja, kwa hivyo wanaowazunguka watajua kinachoendelea kati yenu, pia chochote kuhusu marafiki wa pembeni kitakuwa kina maelezo ya kutosha.

Wivu pia husaidia kuwafanya wahusika kutambua wajibu wao, hivyo kufanya uhusiano kuwa na afya zaidi. Hata hivyo, kuwa na mpenzi (mume au mke) mwenye wivu inakuhitaji zaidi uwe muelewa kuliko kawaida.

sizarinah@gmail.com

You can share this post!

MWANAMUME KAMILI: Ndoa thabiti ni msingi wa familia na...

Bertrand ajiunga na Leicester baada ya kandarasi yake na...