Makala

UMBEA: Si vizuri kuficha hasira, yaweza kugeuka shubiri maishani

March 21st, 2020 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

HASIRA siku zote matokeo yake ni hasara.

Na ndiyo maana hasira na mizozo inapotawala kwenye ndoa ama mahusiano, kuvurugana inakuwa ni kawaida ya kila siku.

Si kila hasira haina mpangilio, na mara nyingi inatokana na mambo ya kiafya, ni hali ya asili inayojitokeza katika mambo tunayokutana nayo.

Njia sahihi ya kukabiliana na tatizo linalokukabili, ambalo linakusababishia hasira, si tu kulenga katika kutafuta muafaka, lakini zaidi ni jinsi gani ya kulichukua na kukabiliana nalo.

Ingawa pia hasira, migogoro na patashika huongeza ladha ya maisha, ladha hii inatakiwa iongezwe kwa kiasi. Inapozidi na kupitiliza huwa sio ladha tena bali ni shubiri inayoweza kuleta madhara.

Kuepuka, kudhibiti ama kuzielewa hasira kunahitaji mbinu. Mbinu ambazo zitakuacha salama, bila ya kujeruhiwa hisia zako.

Mbinu ya muhimu ni jinsi ya kujielewa pale unapokasirika, ujitambue na ujue kwamba hali hiyo imekupata. Kwani usipotambua hivyo, hasira inaweza kukupeleka mbio kama gari bovu kwenye mteremko.

Hasira hujaza kifua, huathiri mzunguko wa damu na ufahamu. Unapokasirika inakuwa vigumu kusikiliza maoni, ushauri ama kutathmini jambo lolote lililo mbele yako. Hasira zinapokutawala unachotaka kuona ni ushindi, iwe kwa maneno ama mapambano.

Katika hali ya namna hiyo, iwapo mtu mwingine atakuja na busara zake na kujaribu kugeuza mtizamo, sio rahisi kueleweka.

Hivyo unapohisi dalili hizi za hasira, mbinu ya kwanza ni kutulia kwanza kabla ya kuchukua hatua yoyote. Hata iwapo aliyesababisha hasira hizo yupo karibu nawe, chagua kutulia kwanza. Ikiwezekana utoke eneo husika na uende mahali ambapo unaweza kukaa kimya kwa muda.

Kutatua matatizo yanayokusababishia hasira kutaleta matokeo mazuri, lakini pia si kujiadhibu mwenyewe kama jibu halitakuja kama ulivyotarajia.

Watu wenye hasira mara nyingi hurukia jambo na kulifanyia maamuzi, lakini baadhi ya maamuzi hayo yanaweza yasiwe sahihi.

Kitu cha kwanza cha kufanya kama upo kwenye majadiliano makali ni kupunguza hasira na kufikiri juu ya majibu yako unayoyatoa.

Wakati unahisi kuwa unataka kuwa na hasira, ni vyema ujifikirie iwapo ungekuwa ni mtu mwenye mamlaka ya juu, ambaye unamiliki mitaa, maduka na maeneo ya ofisi, mwenye maendeleo ya haraka na kuwa na taratibu zako katika hali zote, wengine wanapotofautiana nawe.

Jambo unaloweza kulijua zaidi katika mawazo yako, unajiona kuwa wewe si mtu wa maana, unaanza kuona vitu ulivyonavyo havina umuhimu, hivyo unakuwa na hasira kutokana na ukweli huo.

Wakati mwingine hasira inabadilisha mazingira yako. Kwa mfano mazingira yetu yanafanya kuwe na misuguano pamoja na ghadhabu. Matatizo na majukumu yanaweza kukuongezea uzito na kukufanya upatwe na hasira.

Ipe nafsi yako mapumziko. Hakikisha una muda wako binafsi na ratiba inayokuongoza kwa siku nzima. Mfano ni kwa mama anayefanya kazi, ambaye amekuwa na sheria yake kwamba, wakati anarudi nyumbani kutoka kazini, kwa dakika 15 za kwanza hakuna yeyote atakayezungumza naye, baada ya muda huo mfupi wa mapumziko anajisikia vizuri na kuanza kuwaandalia watoto wake mahitaji yao kwa furaha.

Njia nyingine za kukupa afueni katika maisha yako, ni kuwapo matukio tofauti ambayo yatakuondolea tatizo la hasira ulilonalo.

Watu wengine wanazika hasira zao ndani. Kama unafanya hivi, utapata maumivu ya kichwa au tumbo. Na mara nyingine unaweza kuanza kulia peke yako.

Si vizuri kuficha hasira yako, inakubidi utafute njia ya kuitoa pasipo kujiumiza mwenyewe au kuwaumiza wengine.

 

[email protected]