Na SIZARINA HAMISI
WAKATI nakua kulikuwa na tunda linaloitwa mung’unya.
Tunda hili lilikuwa linaliwa likiwa changa tu, kwani likikomaa halikuwa linalika tena.
Hivyo kama ulitaka kulitafuna tunda lile, ilibidi kuliwahi kabla halijakomaa, kwani likishakomaa lilikuwa linavunwa na kutumiwa kama kata ya maji (kibuyu cha kuchotea maji).
Na hivi ndivyo zilivyo baadhi ya tabia za watu. Basi mwakwetu kuna watu hawana haya, waliopinda tangu udogoni na kujificha katika mavazi ya heshima na maneno matamu, lakini tabia zao ni rangi ya kaniki hata ukifua vipi haiwezi kuwa nyeupe kwa vile weusi ni rangi yake ya asili.
Na hivi leo nitazungumzia tabia za aibu zinazofanywa na wanawake wenzetu walio ndani ya ndoa. Kuna mama mtu mzima ambaye katika hali ya kawaida ilibidi awe mtulivu katika ndoa yake, kwani amekuwa akimdhalilisha mumewe kwa kutembea nje ya ndoa yake na wanaume lukuki bila aibu tena kujiona kufanya vile ni haki yake.
Shoga yangu mmoja ambaye ni jirani yake na ni mtu wake wa karibu sana, alikasirishwa na kuvurugwa na tabia ya yule mama na ndiposa siku moja akamtolea uvivu na kumpasha bayana kwamba anayofanya siyo mazuri anamuaibisha mumewe.
Japo mama huyu mtu mzima anayetakiwa kuwa na wajukuu alisingizia mumewe hamfikishi pale anapotaka, ukweli ni kwamba tabia yake ishakomaa na haikuwa inavutia tena.
Alipoulizwa aliishije na mumewe miaka yote iwapo alikuwa hamshibishi kiasi cha kuamua kugawa mwili wake kama peremende, yule mama hakuwa na jibu la kuridhisha.
Najua nimekugusa na wewe mwenye tabia kama hii, huenda umeshapinda mdomo kama kiatu cha mwanajeshi mstaafu. Kwamba ndiyo tabia yako ya kuugawa mwili kwa wanaume ovyo kama mapokezi ya nyumba ya wageni kila mgeni lazima apitie.
Kwa hili siwezi waacheni mchafue sifa za ndoa. Kama una hamu ya wanaume unaonaje ujitoe kwenye ndoa, ijulikane kwamba shughuli yako ni kugawa huo mwili wako.
Nasema na wewe unayejijua na kujibu majibu ya kifedhuli tena nakwambia uache tabia yako ya kumdhalilisha mumeo. Mbona wenzako wametulia kwenye ndoa zao kwani miili yao wameazima kwa watu?
Inawezekana haya ninayoyasema yataingilia kulia na kutokea kushoto, siwezi kukulaumu kwa vile umeshaharibika ukubwani kama mung’unya na tabia yako kama rangi ya kaniki hata ukimaliza bahari nzima na sabuni zote za duniani bado rangi yako itabakia nyeusi.
Siku hizi makahaba sio tena wa kusimama mitaani ama barabarani, wapo kwenye ndoa, tena ni watu nadhifu na ukiwaona kwa haraka unaweza ukadhani ni maafisa fulani. Ni wazi kwamba makahaba wapo kwenye ndoa na wala sio mitaani tena. Haya ndio mamung’unya ambayo yalikuwa na ladha nzuri yalipokuwa machanga, kabla hayajakomaa, lakini baada ya miaka kadha kwenye ndoa, kukomaa na kujua duniani ni kitu gani, basi yamekomaa na sasa hayashikiki, hayaliki, hayatazamiki, hayavutii, na wala hayapendwi tena.
Na hivyo ili kujinusuru na kupoteza thamani yake mamung’unya haya yanakesha kutwa kucha yakikimbizana na vijana wadogo, wengine wakiwa umri wa vijana wao ili kujiridhisha kwamba bado yanalika. Jiulize, nawe ni mmoja wa mung’unya?