Makala

UMBEA: Unapopenda vitu vizuri, basi kuwa tayari pia kugharimika

October 19th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA usione vyaelea, vimeundwa.

Na ujumbe wa leo uwafikie akina kaka mnaofurahia wasichana warembo, mnaovutiwa na wasichana wanaopendeza kwa mavazi na muonekano, wanaoishi maisha fulani ya kuvutia.

Kwamba unapoona msichana anapendeza na kuvutia, utambue kuna gharama imetumika na huenda yupo yule aliyegharimia kumfikisha hiyo hali nzuri uliyomuona nayo.

Halafu wapo wale akina dada waliojaaliwa maumbile, wenye muonekano matata kiasi cha kumpagawisha mtu bila ya kujitambua.

Hakuna anayependa kitu kibaya na kitu kizuri hupendwa na kuvutiwa na wengi.

Ukitathmini kwa makini utaelewa kwamba baadhi ya akina kaka, hupagawishwa na wanawake wanaojipenda, wanaovaa na kupendeza, wanaonukia vizuri na wanaojiweka na hali ya mvuto.

Pengine ndiyo sababu nyumba ndogo nyingi zinakuwa na sifa hizi na kupelekea urahisi wake wa kuteka akili ya mume wa mtu na akamuacha mkewe wa ndoa na kukimbilia mchepuko.

Kupenda vizuri hakuna ubaya, tena ni vizuri mno. Na ndio maana unapopenda vitu vizuri, uwe tayari pia kugharimia. Isiwe kwamba unamuacha mkeo akiwa na hali mbaya, unashindwa kumtengeneza kimuonekano ili awe vile unavyotaka, lakini kutwa kucha kumezea mate wasichana warembo na waliopendeza.

Unakuwa mtu wa kukodolea macho wasichana wa watu bila ya kutambua kwamba unayo nafasi ya kumtengeneza mke wako au mchumba wako, akawa kama hao anaowatamani huko barabarani, sokoni, kazini na wengine hufikia hata hatua ya kutamani wanawake wanaohudumia kwenye sehemu za starehe.

Hali hii pia imekuwa janga kwa wanawake katika siku za karibuni. Ingawa wao sio rahisi kutamka pale wanapovutiwa na mwanaume aliye mtanashati, aliyejenga misuli, mwenye uwezo kifedha, anayeonyesha kuelewa hisia za mwanamke na labda anayejua kuzungumza vizuri na mwanamke.

Hapa ndipo unakuta dada akiota mchana kwamba siku atakayokuwa na mwanaume huyo, atafanya hivi ama atafanya vile. Na sababu mwanamke huongozwa zaidi na hisia na sio macho, ni nadra kukuta akigeuka na kumwangalia mwanaume mara mbili ama tatu kama ilivyo kwa akina kaka. Lakini atafanya naye udhalimu kifikra na kuota na kufikiria yale yote ambayo katika hali ya kawaida hawezi kuyafikiria kwa mumewe.

Wasichotambua akina dada hawa ni kwamba wanayo nafasi ya kuwatengeneza waume zao vile ambavyo wanatamani. Na matengenezo haya yana jinsi yake, hayafanywi kwa haraka, wala kwa ubabe na wala kwa kulazimisha. Bali hutengenezwa kwa upendo, uelewa na kuwa tayari kuchukua hatua za ziada kufikisha lengo husika.

Baadhi ya wanawake wamesahau kwamba unapokuwa na mume ama mchumba unalo jukumu la kumfanya apendeze na kuvutia, awe kama unavyotaka.

Na kama wewe ni mwanaume, jukumu la kumfanya mkeo au mchumba wako apendeze na kuvutia kama unaowatamani, ni la kwako.

Kubadili mwonekano wa mwenzako hakuhitaji pesa nyingi, bali ni suala la upendo na kujitolea kwako tu kama kweli unampenda na una malengo naye. Iwapo wewe ni mwanamke, hebu jiulize, ni lini ulimnunulia mumeo shati zuri, suruali au hata viatu ambavyo vitamfanya aonekane mwanaume wa kupendeza mbele ya wanaume wenzake?

Kama wewe ni mwanaume, je, unamgharimia mkeo inavyostahili ili aonekane mrembo? Lini ulimpa fedha za kwenda kutengeneza nywele zake vizuri? Lini ulimnunulia mafuta mazuri au nguo nzuri za kumfanya apendeze vile unavyotaka?

Bila shaka majibu utakuwa nayo mwenyewe. Usichangie kuvuruga haiba ya mwenzako kwa kukosa matunzo wakati ukihangaika kutamani wengine wa barabarani. Mtengeneze mwenzako awe jinsi unavyotaka.

 

[email protected]