Makala

UMBEA: Usikurupukie ndoa sababu ya presha ya umri au jamii

July 27th, 2019 2 min read

Na SIZARINA HAMISI

KUNA mwanamuziki fulani wa Tanzania, baada ya kuulizwa ulizwa ataoa lini, aliwajibu waulizao “bado nipo nipo sana.”

Ndoa ni jambo la heri na pia kitu chema na inapaswa kuwa sehemu ya amani na sio maradhi wala vita.

Hata hivyo wengi katika jamii yetu wamekuwa wakiwakera mabinti na akina kaka, hasa wanapotimiza umri fulani kwa swali la utaoa lini ama utaolewa lini.

Tabia hii haifai na tena inakera, kwani kila mtu ana mstari wake wa maisha na haipendezi na wala haileti tija kupanga hatua za maisha ya mtu mwingine.

Hizi kauli za unangoja nini utazeeka, au sijui utakuwa babu, ama sijui nitapata lini wajukuu, ni za kishamba na tena zimepitwa na wakati.

Ndoa sio kitu cha kukimbilia, kitu cha kuiga wala cha kuonyesha watu. Usimshangae au kumshinikiza mwenzako hasa ukijua hajaolewa au kuoa kwa muda unaotaka wewe au unaodhani wewe ni sahihi. Epuka kumpa mtu shinikizo la ndoa kwa sababu wewe uko huko.

Wengi walio kwenye ndoa wanajua kinachowatokea kwa kukurupuka kuingia kwenye ndoa sababu ya shinikizo la jamii. Hivyo basi unapokutana na msichana ama kijana ambaye umri umeenda na hajaoa, usishangae na kutoa mapendekezo yako kuhusu ndoa, kwani huwezi kujua mipango ya maisha yake.

Ndoa sio kitu cha kujaribu kwa kuiga. Ingia kwenye ndoa ukiwa na wito, utayari wa mwili na akili na pia utayari wa uchumi ikiwemo kulea matumbo zaidi ya mawili mwaka mzima bila kukosa kitu.

Hakuna nishani ya ndoa, kwamba ukikimbilia na kuwahi kuoa mapema utapata ushindi na kuvikwa taji. Ndoa ni maelewano ya watu wawili, mwanaume na mwanamke ambao wanaona wanaweza kuishi pamoja kwa kusaidiana, kuheshimiana na kuburudishana.

Haipendezi kuishi kwa mikumbo, kufuata kila lisemwalo bila ya kutathmini na pia tusipende kuwalazimisha watu waishi kwa mitizamo yetu au kulingana na yale tuliyopitia, yawe mazuri ama mabaya.

Kero

Ile tabia yako ya kuuliza uliza mabinti ama vijana wa watu watafunga ndoa lini, ni vyema uidhibiti isiwe ni shida kwa wengine.

Kama mwanaume yuko kamili, hawezi kuambiwa aoe muda fulani wakati yeye mwenyewe anajielewa. Huenda bado hayuko tayari, kiuchumi, kimwili ama hata kiakili, kwamba anaona kabisa bado anahitaji kuonja huku na kutafuna kule kabla hajatulia na mtu mmoja.

Pia kwa akina dada, ndoa inafaa kuwa sehemu ya maelewano na amani, usiolewe sababu ya umri umeenda, kama yupo wako, atakuja tu. Usijilazimishe na kujipendekeza sababu ya shinikizo kutoka kwa shangazi zako, nyanya yako, mama ama baba yako. Ufunge ndoa sababu huo ni uamuzi wako binafsi.

Ukikurupuka kama unakufa kesho, utapata jipu chungu likusumbue mpaka upate kisukari na mapresha alafu ufe taratibu kwa mateso makali.

Maisha ni jinsi unavyojipanga. Ni muhimu ujipange, maisha haya ni kufurahia kila siku ukiwa hai. Ndoa inatakiwa iwe sehemu ya furaha yako na wala sio sehemu ya majanga yako. Inatakiwa ikupe furaha na wala sio karaha.

Usijiweke katika hali ya kuishi kwa kunyanyasika sababu ya umri. Umri wako unakuhusu wewe mwenyewe, ukiamua kuolewa ama kuoa ukiwa nyanya, huo ni uamuzi wako binafsi na hauna budi uheshimiwe.

Uishi kwa furaha maana maisha ni mafupi na ukifa hamna maisha tena. Habari ya leo ndio hiyo!

 

[email protected]