UMBEA: Utandawazi usitutoe fahamu tusahau msingi wa mahusiano

UMBEA: Utandawazi usitutoe fahamu tusahau msingi wa mahusiano

Na SIZARINA HAMISI

WANASEMA usione vyaelea utambue kwamba vimeundwa.

Unapoona wapendanao ama wanandoa wamedumu kwenye uhusiano ama katika ndoa, uelewe kwamba nyuma ya uhusiano huo kuna kazi kubwa imefanyika. Kupata wanandoa wameishi miaka mingi kwa amani na furaha, inamaanisha kwamba wamevumilia na kuepukana na mengi kwani maisha ya uhusiano yana changamoto nyingi.

Na ndio maana katika hali ya sasa, wengi hushindwa kuvumilia na kumudu changamoto za ndoa ama uhusiano na kupelekea ndoa nyingi kuvunjika. Wanakosa uvumilivu na matokeo yake ndoa inayeyuka. Mara nyingi mvurugano huu hutokea sababu ya ujuaji uliokithiri, kila mmoja anapojifanya anajua mambo na wengine kuwa na ujeuri wa mfululizo. Panapo jeuri, maelewano huwa ni magumu kupatikana. Kwani maelewano yanatengenezwa, huwa hayajileti yenyewe. Ili waweze kuishi vizuri, wapendanao wanatakiwa kuvumiliana. Kwani watu wawili wanapofunga ndoa, kila mmoja huja na tabia zake kutoka kwao, hivyo maisha ya pamoja yanapoanza inatakiwa kutengeneza umoja na pia kuvumiliana. Zibebe changamoto za mwenzako kama za kwako.

Iwapo kuna jambo linakukwaza na kweli unaliona linakuletea shida, basi usikurupuke kutafuta suluhu. Tumia muda wako kuona namna unavyoweza kumbadilisha arudi kwenye mstari. Tumia busara na wala sio ubabe, busara na hekina ndizo zinaweza kumbadilisha mwenzako kutoka kwenye jambo ambalo wewe unaamini sio zuri. Ni tabia yake, aliijenga kwa muda mrefu, huwezi kuibadili kwa mara moja kama vile unazima swichi ya taa.

Huna budi kumsoma mwenzako kwamba kuna kipindi anakuwa hayupo sawa. Usilazimishe kufikisha jambo lako siku ambayo unaona hali yake haiko kawaida. Umjue kwa undani kwamba anapovurugwa kazini au kwenye biashara zake anakuwaje. Badala ya kumuongezea changamoto, msaidie kwa kumliwaza. Usichochee moto wa ugomvi wakati anapokuwa hayupo sawa. Kwani kuna wakati anaweza kuwa hajisikii kuzungumza. Si kwamba anataka kukusaliti au kukufanyia jambo lolote baya, lakini hajisikii kuzungumza.

Wazee wetu waliweza kudumu kwenye uhusiano kwa muda mrefu kwa sababu walikuwa na uvumilivu. Waliweza kubebeana changamoto zao. Kila mmoja aliweza kusimama kwenye nafasi yake. Mwanamke alijua wajibu wake kwa mumewe, vivyo hivyo mwanaume. Hakuonyesha jeuri na alimheshimu mumewe. Sasa hivi wanawake wanataka waheshimiwe kama si kusujudiwa na wanaume.

Kwa upande wa wanaume, wazee wetu walikuwa wanajua kuwapenda wake zao. Waliwajali, kuwathamini kupita kiasi kwani walikuwa wanaelewa kwamba mwanamke si chombo cha kuteswa na kupigwa bali kuonyeshwa mahaba. Wazee walielewa kwamba wanawake wanatakiwa kupewa zawadi kama vile vitenge na kadhalika. Mwanamke hata awe na kazi fulani yenye mshahara mkubwa, hapati kiburi kwa mumewe. Anamheshimu kupita maelezo. Hii ndiyo sifa ya wazee wetu kudumu kwenye ndoa. Wao walizibeba changamoto na kutafuta suluhu kwa busara na hekima hata kama kosa ni kubwa kiasi gani.

Utandawazi usitutoe ufahamu na kusahau misingi ya maisha ya uhusiano. Upendo wa kweli, kuheshimiana na uvumilivu ndiyo silaha za kuweza kudumu kwenye mahusiano.

sizarinah@gmail.com

You can share this post!

Corona yasukuma watoto kushiriki katika ugaidi – UN

FATAKI: Unyenyekevu si udhaifu wala haupunguzi hadhi au...