UMBEA: Uvumilivu una kikomo chake, chunga usije ukala zilizooza!

UMBEA: Uvumilivu una kikomo chake, chunga usije ukala zilizooza!

Na SIZARINA HAMISI

ENYI kina dada nishawahi kusema na narudia hivi; kuna wanaume wengine waacheni wapite.

Waende zao kwa amani, wasiwatilie majanga yao kwenye maisha yenu.

Pamoja na ule msemo wa mvumilivu hula mbivu, kuna hawavumiliki.

Uvumilivu unafaa tena ni muhimu katika uhusiano, lakini kuna yale yanayovumilika na mengine hayafai na tena hayana nafasi ya kuvumilika.

Iwapo umetokea kumpenda mtu fulani lakini kwa bahati mbaya ukakutana na tabia ambazo hukuzitarajia, utamuacha?

Hili haliwezi kuwa suala la kukuweka njia panda hata siku moja kama uelewa wako utakuwa mkubwa.

Iwapo umekutana na mwanaume na kila siku ni ngumi na mateke, tafakari iwapo hayo ni maisha utakayopenda kuishi.

Pia kama umekutana na mwanaume muasherati anayekuonyesha wazi jinsi anavyovutiwa na wanawake wengine, bado utavumilia?

Na je kama umekutana na mwanaume mlevi mithili ya komba, kila siku anaokotwa mtaroni, amezimika na kujiachia haja ndogo nguo zikiwa chafu mithili ya mchoma makaa?

Lakini kama utaamua kumvumilia mwenzako kwa matumaini ya kuona mabadiliko, basi katika kipindi hicho jaribu kumueleza namna tabia zake zisivyokufurahisha.

Kama kweli atakuwa anakupenda, nina imani atabadilika.

Hata hivyo ni muhimu kujiwekea maazimio na mikakati katika huo uvumilivu wako.

Ndoa nyingi siku hizi zinadumu sababu ya uvumilivu wa muda mrefu na kuamua kwamba liwalo na liwe.

Kama huamini katika hili, jaribu kuchunguza na utabaini wengi ambao sasa hivi wanaishi maisha ya furaha na amani walivumiliana kwa mengi hadi kufikia hatua uhusiano wao ukasimama.

Kuwa na subira na wala usiwe mtu wa kukata tamaa haraka.

Katika maisha ya sasa, watu hawaeleweki, hakuna unayeweza kuwa na uhakika naye asilimia mia moja kuwa anakupenda kwa dhati, subira yako ndiyo itakufanya ugundue hilo.

Mvumilie mpenzi wako huku ukijaribu mara kwa mara kuzungumza naye, usiwe mwepesi wa kuchukua uamuzi. Kwa upande mwingine, uvumilivu una kiwango chake.

Usiwe ni mtu wa kulizwa kila siku lakini unashindwa kuchukua uamuzi sahihi eti kwa kuwa tu umeambiwa mvumilivu hula mbivu.

Vumilia lakini angalia usije ukala zilizooza badala ya zilizoiva.

Kumbuka si kila mpenzi unayekuwa naye anastahili kuvumiliwa kwa muda mrefu, wengine mapema kabisa wanaonekana hawafai hivyo ni uamuzi sahihi kuwaacha wapite.

sizarinah@gmail.com

You can share this post!

Vigogo Man-U, Chelsea na Liverpool mawindoni leo

Leicester wapata beki wa kuziba pengo la Fofana...