UMBEA: Wakati mwingine mbaya wako ni wewe mwenyewe!

UMBEA: Wakati mwingine mbaya wako ni wewe mwenyewe!

Na SIZARINA HAMISI

KUNA wale wenzangu ambao hubaki wamepigwa na butwaa mambo yanapoenda kombo.

Pale wanapoandamwa na mikiki na patashika za nguo kuchanika.

Kwamba ulimpenda sana mwenzako, naye alionyesha kukupenda kwa dhati, lakini ghafla kakuacha kwenye mataa kaibuka na binti wa mtaa wa pili.

Wakati mwingine mbaya wako ni wewe mwenyewe.

Yaani unaweza kuwa sababu ya kutemwa na mpenzi wako hata kama atakuwa anakupenda sana.

Unapokuwa mtu wa matatizo kila siku, huwa inafika wakati unachosha!

Iwapo unamtegemea sana mpenzi wako, ni rahisi kubadilisha uamuzi wake, kwani ataona wewe ni mwanamke wa kumchuma tu na huna malengo naye na maisha ya baadaye.

Sababu nyingine zinazoweza kumfanya mwenzako akutoroke ni pamoja na;

•Ukorofi: Mara nyingi ukorofi huwa ni chachu katika uhusiano wa kimapenzi. Shida hii inatosha kabisa kukukosesha mpenzi wa kudumu ambaye baadaye anaweza kuwa mchumba na hatimaye kuingia katika ndoa. Jichunguze vizuri je, wewe ni mkorofi? Unaufahamu vipi ukorofi? Hapa tunazungumzia dharau, majibu ya mkato na kutokuwa msikivu. Mwanamke ambaye anatarajia kuingia katika ndoa hapo baadaye na mchumba wake lazima atakuwa makini na ulimi wake, hawezi kumjibu vibaya mpenzi wake kwa kuwa anajua anamjibu mumewe mtarajiwa. Jichunguze vizuri, utagundua kuwa kuna tatizo hili katika uhusiano wako uliopita. Ukorofi mwingine ni kumpangia mwenzako muda wa kuwa naye faragha. Akikuhitaji muda fulani unamkataa na kutoa sababu kibao zisizo na msingi. Ni sawa na kumruhusu mpenzi wako atafute mwanamke mwingine wa nje. Unadhani akifanya hivyo na akikolezwa kimahaba, utampata tena

•Hauonyeshi mapenzi: Naweza kusema kuwa hii ni sababu kubwa zaidi na yenye uzito wa kukukosesha mchumba wa kudumu. Huwezi kuwa na mpenzi ambaye huna uhakika kama ana mapenzi ya kweli na wewe au anakulaghai. Njia mojawapo ya kuonyesha kuwa ni kweli mpenzi wako unampenda kwa dhati ya moyo wako na siyo kujilazimisha ni kuonyesha mapenzi ya kweli. Hebu jiulize, unaonyesha mapenzi kwa mwandani wako? Swali hili linawahusu wote, yaani wanaume na wanawake, walio ndani ya ndoa na wachumba. Sijui kama naeleweka vyema ninaposema kuonyesha mapenzi kwa mwandani wako. Hapa kuna mambo mengi ikiwemo mashamsham na kuonyesha kuwa huna kinyaa kwa mpenzi wako. Mwingine hata kumbusu mpenzi wake inakuwa shughuli. Sasa kama hata kumbusu tu mpenzi wako unashindwa, jiulize iwapo una mapenzi kweli. Utakuta mwingine akiwa faragha anashindwa kumridhisha vyema au hataki kushiriki na mwenzake, huyu atakuwa anahitaji nini kama siyo kuachwa?

•Ushauri wa bure: Kama una nia ya kuwa na mume hapo baadaye, lazima utulie na uishi kama mwanamke mwenye malengo na mapenzi ya dhati. Achana na tabia za mtaani, usisikilize ushauri mbaya wa marafiki. Onyesha mapenzi ya kweli, mheshimu mchumba wako maana huyo ndiye atakuwa mume wako hapo baadaye. Uamuzi wa kuolewa au kumpa mshawasha mpenzi wako wa kukuoa upo mikononi mwako na bila shaka unaweza! Kumbuka kwamba, hakuna sheria maalum katika mapenzi. Inahusu zaidi uwazi wako, utayari wa kumkubali mwenzako kama alivyo, kuwa tayari kwa changamoto ambazo huambatana na uhusiano ama maisha ya pamoja na wakati mwingine kuwa tayari kutenda yale ambayo hujisikii kuyatenda ili kumfurahisha ama kumridhisha mwenzako.

sizarinah@gmail.com

You can share this post!

CHOCHEO: Ukitunzwa, jitunze!

AIK anayochezea Mkenya Eric ‘Marcelo’ Ouma...