Michezo

Umeme Bees yakosa taji la Koth Biro

July 31st, 2019 1 min read

Na JOHN KIMWERE

MATUMAINI ya Umeme Bees FC kushiriki fainali ya kipute cha Koth Biro makala ya 41 yaligomba mwamba iliponyamazishwa kwa bao 1-0 na Kingstone FC kwenye nusu fainali iliyochezewa Ugani Umeme Ziwani, Nairobi.

Nayo MASA ilijikuta kwenye wakati mgumu ilipolimwa kwa goli 1-0 na Allin Jua Kali FC inayoshiriki ngarambe hiyo kwa mara ya kwanza. Timu za Umeme Bees FC na Kingstone FC kila moja ilishusha ushindani mkali huku pande zote zikishambulia kutafuta tiketi ya kusonga mbele.

Wachezaji wa Umeme Bees walijitahidi kwa udi na uvumba lakini wapi walikosa ujanja pale Crispinus Onyango alipotingia Kingstone FC bao la ushindi dakika ya 90.

Wafuasi wa Umeme Bees waliondoka katika ardhi ya nyumbani shingo upande baada ya kuaibishwa na wachezaji hao.

Naye Victor Otieno alitikisa wavu mara moja na kubeba Allin Jua Kali FC kunasa tiketi ya fainali ya mwaka huu. ”Nashukuru wachezaji wangu kwa kuonyesha ukakamavu tosha na kusonga mbele kushiriki fainali ya mwaka huu,” kocha wa Allin Jua Kali FC, Thomas Okongo alisema.

Kwenye robo fainali za ngarambe hiyo, Kingstone FC ilikomoa Ping FC kwa magoli 2-0, Allin Jua-Kali ililaza Napoli FC mabao 2-0 nazo Umeme Bees na MASA kila moja ilivuna ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Nyoi FC na Dallas FC mtawalia.

Bingwa wa kinyang’anyiro hicho kinaofadhiliwa na Sportpesa kwa mara ya tatu mfululizo atatuzwa Sh300,000 nayo timu itakayoibuka ya pili itatia kibindoni Sh100,0000.

Kisha tuzo ya Sh50,000 na Sh25,000 itaziuendea timu zitakaomaliza nafasi ya tatu na nne mtawalia.