Makala

UMEME KWA WOTE: Bei ghali yazidi kulemaza mpango

May 29th, 2018 3 min read

Na VALENTINE OBARA

BI ANNE Mueni ni mfanyabiashara anayemiliki hoteli katika eneo la Burani, Kaunti ya Kwale, ambaye ameamua kutegemea kawi ya sola hata ingawa kuna miundomsingi ya kuunganishiwa umeme katika eneo hilo.

Katika miaka sita ambayo amefanya biashara hiyo, Bi Mueni anasema ameshuhudia kuna manufaa zaidi katika kutegemea kawi ya miale ya jua kuliko umeme wa kawaida ambao hupotea mara kwa mara.

“Awali nilikuwa ninatumia stima lakini nikaamua kubadilisha na kuanza kutumia sola. Kwanza, vifaa vya sola vinahitaji tu kulipiwa kwa muda kisha unavimiliki. Pili, katika eneo hili huwa stima zinapoea kila mara. Unaweza hata kukaa wiki nzima bila stima,” akaambia Taifa Leo.

Mfanyabiashara huyo alinunua vifaa vyake kupitia kwa mpango wa shirika la M-Kopa ambalo huwapa watu nafasi ya kununua vifaa vya sola kwa mkopo.

Yeye ni miongoni mwa maelfu ya Wakenya vijijini ambao wanaamua kuwekeza katika vifaa vya sola kutokana na jinsi umeme unaosambazwa na shirika la Kenya Power unavyopotea mara kwa mara, na pia kutokana na gharama ya juu ya huduma hizo za umeme.

Kwa miezi kadhaa mwaka huu, Wakenya katika maeneo mbalimbali walilalamikia gharama ya juu ya umeme ambayo pia haiwezi kutegemewa kikamilifu. Hili ni tatizo ambalo limekuwepo kwa muda mrefu, ingawa sasa inaonekana wananchi wamechoshwa nalo.

Wiki chache zilizopita, Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o alitoa changamoto kwa serikali kuu iruhusu mashirika mengine kuingilia biashara ya usambazaji umeme kwani anaamini matatizo yaliyopo yanatokana na jinsi shirika moja pekee ndilo linafanya biashara hiyo bila ushindani.

“Stima hupotea sana kupita kiasi Kisumu. Hali hii huathiri watumizi manyumbani, katika viwanda na kwingineko,” akasema alipohutubu kwenye mkutano wa kila mwaka wa Shirikisho la Waajiri wa Kenya.

Katika eneo la Moyale, Kaunti ya Marsabit, wakazi waliamua kuandamana ili kuonyesha ghadhabu yao dhidi ya kupotea kwa stima mara kwa mara.

Malalamishi haya ya bei ghali ya umeme na kupotea kwa stima kila mara sasa yameibua wasiwasi kuhusu kama serikali itafanikiwa kutimiza malengo yake ya kuwezesha kila mwananchi kufurahia manufaa ya kuunganishiwa umeme.

Tangu mwaka wa 2015, serikali kupitia kwa mpango wa ‘Last-Mile’ imekuwa ikiunganishia wananchi mashinani na vijijini umeme kwa bei nafuu. Mpango huu ni miongoni mwa malengo makuu kwenye Ruwaza ya 2030.

 

‘Asilimia 71 wana umeme’

Katika hotuba yake kuhusu Hali ya Taifa aliyotoa bungeni mapema Mei, Rais Uhuru Kenyatta alisema mpango huo unaofadhiliwa na serikali kwa ushirikiano na Banki ya Maendeleo ya Afrika umefanikiwa kuongeza idadi ya nyumba zilizounganishiwa umeme kutoka asilimia 27 katika mwaka wa 2013, hadi asilimia 71.

“Ninajivunia sana mafanikio ya mpango huu kwa sababu ninajua mabadiliko yanayoleta. Nimejionea kibinafsi kwamba siku ile familia inapowasha taa kwa mara ya kwanza, maisha yao yote hubadilika,” akasema.

Hata hivyo, imebainika kwamba kuunganishiwa umeme pekee hakuna manufaa ikiwa huduma zitakuwa duni na za bei ghali.

Kulingana na ripoti ya Benki ya Dunia iliyotolewa hivi majuzi, uwezo wa wananchi kugharamia umeme ni jambo muhimu katika kufanikisha usambazaji wa umeme kwa kila mwananchi. Hili ni lengo la saba katika Malengo ya Ustawi wa Maendeleo (SDG) yaliyoekwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Ripoti ya utafiti huo uliofanywa na Benki ya Dunia kwa ushirikiano na UN, Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) miongoni mwa mashirika mengine ilitolewa Mei 3.

“Imebainika kuwa hata katika mataifa ambayo yamefanikiwa kusambaza umeme kwa kila mwananchi, bei ghali ya umeme huathiri karibu asilimia 30 ya wananchi wao. Katika mataifa ambayo bado yanajitahidi kufikisha umeme kwa kila mwananchi, suala hili huathiri asilimia 57 ambao wamefikiwa,” ikasema ripoti hiyo.

 

Sera ya kupunguza bei 

Aliyekuwa Mkurugenzi wa Ruwaza ya 2030, Bw Mugo Kibati, alisema inahitajika taifa liwe na sera ambazo zitawezesha walio masikini katika jamii kupata kawi safi kwa njia wanayoweza kugharamia.

Kwenye mahojiano aliyofanyiwa na wanahabari Nairobi, Bw Kibati ambaye pia ni Mwenyekiti wa kapuni ya M-Kopa alisema ingawa mpango wa Last-Mile una nia njema ya kuinua hali ya maisha kwa wananchi wote, ni muhimu kutafuta suluhisho ambazo wale wanaolengwa wataweza kugharamia kwa muda mrefu.

“Sehemu kubwa ya Last-Mile inahusu kupunguzia wateja bei ili kuwawezesha kuunganishiwa umeme. Lakini kwa kutumia pesa kidogo zaidi kuliko zilizotumiwa katika mpango huu, tunaweza kupata manufaa zaidi kutokana na mbinu watakazoweza kugharamia kwa muda mrefu,” akasema, akiashiria uwekezaji kwa kawi ya miale ya jua.

Kwenye bajeti ya mwaka huu, serikali imepanga kuwekeza katika mbinu tofauti za kuzalisha kawi mbali na kutegemea mabwawa ambayo yamedhihirika hayawezi kutegemewa kikamilifu. Miongoni mwa mbinu mbadala zilizotambuliwa ni mvuke, upepo na sola.