Umetuvunjia heshima, wasusi wamfokea Boniface Mwangi

Umetuvunjia heshima, wasusi wamfokea Boniface Mwangi

NA WANGU KANURI

Ususi ni tajiriba ambayo imewasaidia wengi kujichumia riziki na kujiendeleza kimaisha. Isitoshe, sanaa hii ambayo inaendelea kukua huku mitindo geni ikichipuka kila kuchao, imewafanya wasusi kujitosa katika mabadiliko yajayo ili kubaki kwenye soko.

Shule ambazo hufunza taaluma hii ya ususi pia, zimekuwa zenye kuyapokea mabadiliko yajayo haswa kwa kuiga mitindo ya nchi za bara. Japo kuna wasusi ambao huenda shuleni ili kupata ujuzi huu, wengine hujifunza manyumbani kupitia mitandao ya kijamii kama Pinterest na YouTube na wengine wakifunzwa na wale wapo kwenye kazi hii.

Kazi hii ya ususi huhitaji bidii na ukakamavu mwingi ili kuhakikisha kuwa mteja amesukwa staili aliyotaka. Isitoshe, msusi hulazimika kusimama kwa muda mrefu katika kutekeleza kazi yake.

Aidha, ili kuwavutia wateja wengine, kazi ya mikono yao ndiyo tegemeo na njia pekee ya kuikuza biashara hii mahususi. Japo wengi wanaweza kuipuuza kazi hii na kuinasabisha kama kazi ya kijungu jiko, ulimbwende na utanashati wa mtu huwa na asilimia kubwa inayotegemewa na umaridadi wa kichwa cha mtu husika.

Hata hivyo, mwanaharakati na mwenye kupigania sana haki za wanadamu, Boniface Mwangi, aliidunisha kazi hiyo aliposema kuwa iwapo gavana wa Mombasa Ali Hassan Joho akijiunga na kazi hii ataharibu biashara.

“Wasusi wamesema @HassanAliJoho akiwaunga ataharibu biashara. Hawataki watu wazembe kwa kazi yao,” Boniface Mwangi akaandika kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Matamshi yake yalikuwa kama kejeli kwake gavana huyu kwani Joho anakimezea mate kiti cha urais. Kwake Boniface, Joho anaweza tu kuwa msusi au mvuvi, akasema kwa kicheko.

“Huyu mwanamume amewafeli watu wa Mombasa kwa sababu alimsaidia Uhuru katika kuhamisha uidhinishaji na usambazaji wa bidhaa kutoka bandari ya Mombasa hadi Naivasha. Hatua hii iliwafanya watu wengi wa Mombasa kukosa kazi. Alichaguliwa kuwawakilisha watu wa Mombasa lakini kazi yake imegeuka kuwa utapeli na kujionyesha kupitia mitandao ya kijamii. Amezoea kuringa tu kuhusu alivyotengeneza pesa na hivi kusahau kazi yake. Anarandaranda tu na wasichana wadogo. Anaweza kuwa mvuvi ama msusi. Hebu fikiria mkimchagua msusi kuwa rais wenu?” akauliza kupitia video katika ukurasa wa Twitter.

Matamshi yake yaliibua gumzo kwenye mitandao ya kijamii huku wakenya wakisikitishwa kwa kuvunjiwa kwa heshima kwa wasusi. Hashtegi ya #shameonyouboniface ikikwea juu ya hashtegi za siku ya leo huku msusi mmoja mwenye tajriba ya ususi na mwenye kuwalea wengi akiwaeleza aliowalea kuwa Boniface Mwangi asinyolewe kwa mwaka mmoja. Hii ikiwa kama njia ya kumwadhibu.

“#shameonyouboniface Lazima uombe msamaha kwa wasusi wote na wataalamu wote nchini kwa kututusi na kutudunisha. Kivipi wanaharakati wanaweza jishusha namna hii? Akauliza @Jeff_njeff.

“Huyu Boniface Mwangi anajiona na kujitambua sana kiasi cha kudharau kitenga uchumi cha wengine. Je, wanajua ni wakenya wangapi wanajikimu kimaisha kupitia ususi. Anaweza kisia tu vile tutaonekana iwapo watu hawangenyoa nywele yao? Anapaswa kuomba msamaha haraka iwezekanavyo. #shameonyouboniface,” akatamatisha @MugambiKimathiM.

“Yenyewe maoni kwenye mitandao ya kijamii ni dhana tu. Sasa mimi kama kinyozi nikose kumnyoa Boniface Mwangi akija kwangu kwa sababu ilisemekana asinyolewe? Tafadhali tuweni madhubuti kimaisha,” akaandika @KivuvaFred.

“Ombi la msamaha linahitajika kwa wasusi,” akaandiak @Alemtetezi.

“@Boniface ninafikiri kuwa unatumia kitu ambacho kinadhuru akili yako…. Sijakuzoea na ufala sampuli hii! Sisi wasusi tunaweza kuwa chochote tukitakacho. Unapaswa sana kuomba msamaha!” akaandika @Sirjohn23071841.

“Hii ni jambo la haya sana kuwadunisha wasusi. Unapaswa kuomba msamaha kwao sababu huwaandii chakula mezani mwao. Sisi pia ni viongozi wakuu. #apologisetohairdressers,” akanakili @Terynturibi.

You can share this post!

Watu 4 wa familia moja waangamia ajalini

‘Firirinda’ yapata umaarufu wa kipekee lakini...