Habari

Umoja wa Nasa 'wafufuka' katika mkutano wa BBI Mombasa

January 25th, 2020 1 min read

Na CHARLES WASONGA

MKUTANO wa kutoa uhamasisho kuhusu ripoti ya mchakato wa maridhiano (BBI) uliofanyika Jumamosi mjini Mombasa kwa mara kwanza ulionekana kurejesha umoja katika muungano wa upinzani (Nasa).

Kwa mara kwanza tangu msururu wa mikutano hiyo ilipoanza mjini Kisii mapema Januari, vinara watatu wa muungano huo, wakiongozwa na kiongozi wa ODM Raila Odinga walishiriki jukwaa moja katika bustani ya Mama Ngina Waterfront.

Na ingawa mkutano huo ulihudhuriwa na viongozi wa kisiasa kutoka mrengo wa Jubilee, hata ule wa ‘Tangatanga’, walioongoza ratiba ya wanenaji walikuwa ni wabunge wa ODM Abdulswamad Nassir (Mvita,) na Junet Mohamed (Suna Mashariki).

Mbw Odinga, Kalonzo Musyoka (Wiper) na Moses Wetang’ula walikariri kuwa mpango wa BBI ndio utakaoleta mageuzi ambayo wamekuwa wakipigania kwa siku.

“Treni ya BBI imeondoka kituo na hakuna kurudi nyuma. Sharti tuwe wakakamavu ili tuweze kufanikisha malengo ya mpango wa maridhiano; lazima tuwe wagumu kama simba ndani ya Zion,” akasema Bw Odinga akiiga wimbo mdundo wa Reggea.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka alituma salama za kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi ambaye yuko nchini Uingereza.

“Nimeleta salama za mwenzetu Musalia Mudavadi, maarufu kama Mdvd ambaye yuko safirini nchini Uingereza. Je, mmepokea?” akauliza.

Bw Musyoka alitumia fursa hiyo kuwatambua wabunge, maseneta na madiwani wa Wiper na kumpigia debe Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo kumrithi Gavana Ali Hassan Joho.

Kiongozi huyo wa Wiper hakudhuria mikutano miwili ya kwanza iliyoafanyika mjini Kisii (Januari 10) na mjini Kakamega (Januari 18).

Lakini Mbw Wetang’ula na Mudavadi walihudhuria mkutano wa Kakamega dakika za mwisho baada ya kutisha kuususia wakilalamikia kutoshirikishwa katika maandalizi yake.