Michezo

Umoja yasajili wanavikapu 3

June 6th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KIKOSI cha Umoja kinachoshiriki Ligi ya Shirikisho la Vikapu la Kenya (KBF) kimejinasia huduma za wachezaji watatu kwa minajili ya kampeni za msimu ujao.

Kwa mujibu wa Steve Kuta ambaye ni kocha msaidizi wa Umoja, kikosi hicho cha kujidhamini kinatarajia kujisuka hata zaidi katika kipindi hiki ambapo shughuli zote za michezo zimesitishwa humu nchini kwa minajili ya kurejelea kampeni za muhula ujao kwa matao ya juu.

Kati ya sajili wapya ambao kwa sasa wanatarajiwa kufufua makali ya kikosi cha Umoja ni Wieu George, Ferdinand Otieno na Shema Nicolas ambao Kuta ameshikilia kwamba wataboresha viwango vya ushindani kambini.

Umoja, ambao walishindwa kufuzu kwa hatua ya mchujo katika kampeni za vikapu msimu uliopita, wamemkaribisha tena Jason Sakwa aliyekatiza uhusiano wake na klabu ya PBC Eastgate.

“Tunalenga kutinga raundi ya pili ya mchujo katika kampeni za muhula ujao. Tunatarajia pia kuwapa chipukizi wetu nafasi maridhawa zaidi ya kudhihirisha ukubwa wa uwezo wao uwanjani,” akasema Kuta.

Kikubwa zaidi kinachomwaminisha kwamba watafaulu katika mengi ya maazimio yao ni kwamba Umoja hawajapoteza huduma za mwanavikapu wao yeyote muhula huu na uwepo wa mseto wa chipukizi na wachezaji wazoefu utakuwa kiini cha kutamba kwao.

“Tunajivunia chipukizi ambao tunaamini watashirikiana vilivyo na wachezaji walio na tajriba pevu katika ulingo wa vikapu. Viwango vya ushindani vitaimarika na matokeo yetu kuboreka,” akaongeza.