Jamvi La Siasa

Umuhimu wa makongamano ya Limuru kwa siasa za taifa

May 17th, 2024 4 min read

NA MWANGI MUIRURI

KONGAMANO la kwanza la wadau wa Mlima Kenya kisiasa lililoandaliwa Machi 12, 1966, na kuitwa ‘Kongamano la Limuru’ liliandaliwa na wandani wa Hayati Mzee Jomo Kenyatta ambaye alikuwa Rais wakati huo.

Inadaiwa wandani wa Mzee Kenyatta walikuwa na ushirika na mwanasiasa wa Luo Nyanza, marehemu Tom Mboya.

Katika kitabu chake David Goldsworthy kinachoitwa ‘Tom Mboya the Man Kenya Wanted to Forget’, kumbukumbu za siasa za Limuru zimeelezewa vizuri na ambapo aliyekuwa mkuu wa kiutawala katika serikali za tangu uhuru Bw Joseph Kaguthi alithibitisha kwamba ni maelezo ya uhakika kama yalivyosukwa.

Afisa mstaafu wa idara ya ujasusi nchini, enzi zake ikifahamika kama NSIS– kwa sasa ni NIS–naye alisema huo ni ukweli, japo akasema tusimtaje jina kwa sababu hili ni suala nzito kwake.

“Soma hicho kitabu na usiniulize maswali. Yale utakayokumbana nayo katika kitabu hicho ni ukweli mtupu na Mungu Akusaidie kudadisi hali ya wakati huo, ya Limuru I na haya sasa ya Limuru III,” akasema afisa huyo mstaafu.

Katika maelezo hayo, kundi hilo la Mboya likiwa ndani ya chama tawala cha Kanu—chama ambacho kilikuwa kimebuniwa mwaka wa 1960—lilikuwa na maveterani kama Charles Njonjo, Njoroge Mungai, Mbiyu Koinange, James Gichuru na Julius Gikonyo Kiano.

Inadaiwa nia yao kuu ilikuwa kudhibiti mamlaka ya utawala na urithi wa Ikulu katika siku za baadaye.

Katika mrengo mwingine kulikuwa na Makamu wa Rais Jaramogi Oginga Odinga (wa kwanza) ambaye kwa ushirika na wanasiasa kama Bildad Kagia, Joseph Murumbi na Paul Ngei, walikuwa wakipanga mkondo mbadala na ukipinga haswa mtindo uliokuwa umechipuka wa wanasiasa fulani kujipa mashamba makubwa yaliyokuwa yakirejeshwa na wakoloni huku wananchi wanyonge wakibakia kuwa mashahidi wa keki ya uhuru ikimegwa pasipo kuwahusisha.

Ni katika kuchunga masilahi ya urais na ukusanyaji wa mali ambapo kundi hilo la Agikuyu lilitekeleza bidii ya mchwa na kuishia kuandaa Kongamano la Limuru na ambapo maafikiano yaliishia kutangaza kwamba Mlima Kenya ungesimama na Mzee Kenyatta na katika siku za usoni za urithi, waongee kwa sauti moja.

Kongamano hilo la Limuru liliandaliwa kama la kamati ya wajumbe wa chama cha Kanu—likiwa ni kongamano la pili la Kanu tangu chama hicho kibuniwe mwaka wa 1960.

Licha ya Oginga kupinga, kongamano hilo lilifanyika na likaishia kumkata miguu pakubwa ambapo wadhifa wake wa naibu makamu wa Kanu ulifutiliwa mbali na badala yake kukaundwa nafasi za wawakilishi wa mikoa minane iliyokuwepo wakati huo.

Katika mkoa wa Nyanza, Lawrence Sagini alichukua nafasi ya Oginga.

Baada ya kusaidiwa na Mboya kupigana na uasi wa Oginga, mwanauchumi huyo alipigwa risasi mnamo Julai 5,1969, mchana peupe jijini Nairobi kwenye barabara iliyoitwa Government Road wakati huo (kwa sasa Moi Avenue.

Mboya aliuawa akiwa na umri wa miaka 39.

Mboya alikuwa ametembelea duka la dawa la Chaani na katika uchunguzi uliozinduliwa, mshukiwa Nahashon Isaac Njenga alitiwa mbaroni na akaishia kuhukumiwa kifo kwa mauaji hayo.

Ni kutokana na maafikio ya Limuru ambapo misimamo mikali Mlima Kenya ilipenyezwa kama ya kuwapa kiapo wenyeji kuwakanya wasiwahi kushirikiana na jamii nyingine kisiasa na wasiwahi kukubali urais uwatoke.

Katika kongamano la Limuru II la Machi 23, 2012, nia ilikuwa ya kuwaweka Agikuyu katika kapu moja la uchaguzi wa 2013 na ambapo iliafikiwa kwamba Uhuru Kenyatta wakati huo akiwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Fedha kwa wakati mmoja, ndiye alikuwa nyota ya jamii hizo za Mlima Kenya ambazo ni Agikuyu, Aembu na Ameru.

Kongamano hili liliishia kuwa na awamu ya pili iliyofahamika kama Limuru II(B) mnamo Aprili 17, 2012, ambapo Bw Kenyatta alithibitisha kwamba alikuwa ameafikiana na William Ruto kuwania urais wa 2013.

Ni wakati huu wa Limuru II (B) ambapo vijana wa kundi haramu la Mungiki likiongozwa na mwenyekiti wao wa wakati huo Bw Maina Njenga waliripotiwa kuvamia eneo la mkutano na kujaribu kuusambaratisha, hali ambayo iliishia wazee wa kijamii kutishia kumlaani Bw Njenga. Uasi huo ulisita mara moja.

Siasa zilizoanza kutokana na Limuru II na Limuru II(B) ziliingia doa wakati aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani George Saitoti na ambaye alikuwa ametangaza nia ya kuwania urais aliaga dunia katika mkasa wa ajali ya ndege mnamo Juni 10, 2012.

Kwa sasa, kongamano la Limuru III ambalo limezua sokomoko linashirikishwa na walio katika mrengo wa Azimio La Umoja-One Kenya katika ukanda wa Mlima Kenya na wametoa kaulimbiu zao kuwa nia yao kuu ni kushinikiza utawala wa Rais Ruto kukoma ‘tamaa’ ya kukata watu na biashara ushuru kiholela bila kujali faida na hasara.

Aidha, wanasema wanataka eneo la Kati liwe likipewa mgao wa rasilimali kwa kuzingatia idadi ya watu na pia maeneobunge ya eneo hilo yakadiriwe upya kimpaka ili kuyazawazisha na mengine yaliyo na idadi ndogo ya watu.

Aidha, baadhi yao wanasema kwamba wanataka kuunda chama kimoja kikubwa cha kisiasa, hali ambayo imezua mtafaruku. Kinara wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Bw Kimani Ichung’wah ambaye pia ni mbunge wa Kikuyu (United Democratic Alliance ndani ya muungano tawala wa Kenya Kwanza) akitaja maazimio hayo kama ya kikabila, yasiyo na msingi na ambayo yanafaa kutatuliwa kwa utaratibu wa sera na sheria.

Kuna wadadisi wanaosema kwamba mrengo huo wa Limuru III uko na nia ya kuzindua mikakati ya kurejesha urais katika jamii hiyo baada ya Rais Ruto kuchomoka nao katika uchaguzi mkuu wa 2022 hivyo basi Bw Ichung’wah kulia kwamba ni njama ya kikabila ambayo inawaongoza waandalizi.

Aliyekuwa Spika wa Kaunti ya Kiambu Bw Stephen Ndichu amekiri kwamba “sisi tukiwa na kura 8 milioni hatufai kuwa ndio tunaongozwa bali tunafaa kuwa wa kutoa mwelekeo wa siasa kitaifa”.

Jambo kuu la kutilia maanani kwa mujibu wa mahojiano na waandalizi wa Limuru III ni kwamba, makongamano hayo yote yanahusishwa pakubwa na familia ya Kenyatta ambapo la kwanza yeye Mzee Kenyatta ndiye alikuwa Rais, la pili na la pili (B) likiwa la Uhuru Kenyatta huku nalo hili la tatu akisemwa, ingawa kinara wa Narc Kenya Martha Karua anakanusha kwa niaba yake, kwamba ni yeye tu mwenye mkoba wa ufadhili.

[email protected]