Makala

Umuhimu wa mkulima kumiliki kipimio chake

August 24th, 2019 2 min read

Na SAMMY WAWERU

SUALA la mawakala kupunja wakulima si geni nchini Kenya.

Isitoshe, mawakala ambao wanaaminika kuwa ‘daraja’ kati ya mkulima na soko, wanalaumiwa kuchangia kudorora kwa bei za bidhaa, mazao na hata huduma.

Katika visa vingi, wafanyabiashara hawa ndio waamuzi wa bei shambani na katika masoko.

Linaloacha mkulima kuuguza majeraha ya hasara, liite “kuamua namna mazao yatapimwa”.

Kwa zaidi ya miaka 20 katika sekta ya kilimo, kero ya mawakala nusra izime jitihada za mkulima Erastus Muriuki.

Ni mkulima wa nyanya na maharagwe aina ya French beans katika Kaunti ya Kirinyaga.

“Hasa nyanya, wakulima wamehangaishwa na mawakala katika upakiaji na bei. Wao ndio huamua mazao yatakavyopakiwa yatakavyonunuliwa,” analalamika Muriuki.

Mkulima huyu anapendekeza makali ya mswada wa mazao, 2019, uliopitishwa na bunge la kitaifa Mei 2, na ambao umeanza kutekelezwa katika uzalishaji wa viazi nchini, uelekezwe kwa nyanya.

Kwa sasa viazi havipakiwi kwa magunia ya kilo 110, mswada huo ukivitaka viekwe kwa kilo 50.

Ili kuepuka kero ya mawakala na changamoto wanazokumbana nazo, wakulima wanashauriwa kujihami kwa vifaa vya kupima mazao.

Mkulima wa mboga za kienyeji Kaunti ya Nairobi Bw Willington Baraza  anasema iwapo kuna kifaa asichokosa shambani ni kipimio.

Ni hatua ambayo imemsaidia pakubwa kujipimia mazao.

“Ukiwa na kipimio chako itakuwa rahisi kuamua bei. Mazoea ya mabroka (akimaanisha mawakala) kukandamiza wakulima yatatatuliwa kila mmoja akikumbatia hili,” anashauri Baraza.

Bw Baraza hukuza mboga za kiasili kama vile kunde, mchicha na mnavu.

Kauli yake inaungwa mkono na Judith Nduva wa kutoka Kajiado.

Judith hukuza mboga za kienyeji sawa na Bw Baraza.

Mkulima huyu pia hukuza spinachi, giligilani, nyanya na vitunguu.

Kulingana na Bi Nduva, mkulima kuwa na kipimio chake huenda sambamba na mkulima asiyekosa jembe shambani.

“Yeye ndiye mwamuzi wa yanavyopaswa kupimwa mazao na hata bei,” anasema.

Katika jukwaa hilo, wataalamu wanapendekeza umuhimu wa kuweka rekodi na kumbukumbu.

“Kuna rekodi za aina mbalimbali, kama vile; gharama, kiwango cha mazao, mauzo na faida. Rekodi zitamuwezesha kujua ikiwa anapata faida au hasara,” anaeleza mtaalamu Harry Thuku.

Mdau huyu pia anahimiza rekodi zijumuishe aina ya pembejeo; mbegu, mbolea na dawa dhidi ya magonjwa na wadudu, pamoja na nambari za simu za wateja na wanakotoka.

Kwa upande wake mtaalamu Daniel Mwenda, mkulima anapaswa kuwa na njia mbadala kutafutia mazao soko kama vile kutumia mitandao.

“Akishapima na kupakia mazao, anaweza kuchapisha katika makundi ya kilimo na wateja kwenye mitandao kama vile Facebook na WhatsApp,” anaeleza.

Pia, anashauri haja ya kujiunga na vyama vya ushirika ambavyo hujizatiti kutafutia wakulima soko katika kiwango cha kitaifa na hata kimataifa.

Njia nyingine ni wakulima kuungana kwa makundi na kushawishi serikali kupitia idara husika kuwatafutia soko la mazao.