Kimataifa

UN yakerwa na video ya ngono

June 27th, 2020 1 min read

CHARLES WASONGA na MASHIRIKA

UMOJA wa Mataifa (UN) umeelezea kukerwa na video moja inayoonyesha mwanamume katika kiti cha nyuma cha gari akishiriki ngono na mwanamke nchini Israel.

Katika video hiyo ambayo ilizungushwa mitandaoni, mwanamke mwenye nguo nyekundu anafanya mapenzi na mwanamume mmoja katika kiti cha nyuma cha gari leupe lenye alama za UN.

Inadaiwa kuwa video hiyo ilinaswa katikati mwa jiji la Tel Aviv.

UN ilisema inachunguza kisa hicho na inakaribia kuwatambua walioko katika video hiyo.

Inaaminika kuwa wahusika ni wafanyakazi wa kikosi cha wanajeshi wa kulinda amani nchini Israeli, umoja huo ulisema.

Stephane Dujarric ambaye ni msemaji wa Katibu Mkuu wa UN Antonio Guterres, alitaja kitendo kinachoonekana katika video hiyo kama “kisichokubalika”.

“Mwenendo huo unaenda kinyume na juhudi zetu za kupambana na utovu wa nidhamu miongoni mwa wafanyakazi wa UN,” akasema Bw Dujarric.

Msemaji huyo alisema uchunguzi unaendelea kubaini ikiwa kitendo hicho cha kufanya mapenzi kilikuwa cha hiari au kilihusisha malipo.

Umoja wa Mataifa umeweka sheria kali inayopiga marufuku vitendo haramu vya ngono miongoni mwa wafanyakazi wake wanaolinda usalama katika mataifa mbalimbali ulimwenguni.

Wafanyakazi wanaokiuka sheria hii huadhibiwa kisha wakarejeshwa katika mataifa yao na kupigwa marufuku kushiriki shughuli za kulinda amani chini ya mwavuli wa UN.

Vilevile, ni wajibu wa mataifa ya washukiwa kuwachukulia hatua zingine za kinidhamu na za kisheria.