Kimataifa

UN yatumai mkataba mpya wa amani utatuliza Darfur

September 27th, 2020 2 min read

Na MASHIRIKA

NEW YORK, Amerika

UMOJA wa Mataifa (UN) umeelezea matumaini kuwa mkataba mpya wa amani kati ya serikali na makundi ya wapiganaji utaleta enzi mpya ya utulivu katika eneo la Darfur nchini Sudan.

Hata hivyo, katibu anayesimamia Operesheni za Amani katika UN Jean-Pierre Lacroix, Ijumaa alisema mengi bado yanapasa kufanywa na pande hizo mbili ili amani ya kudumu iweze kurejea katika eneo hilo ambalo limeshuhudia mapigano kwa miaka mingi.

Lacroix aliambia Baraza la Usalama la umoja huo kuwa mkataba wa amani uliojadiliwa jijini Juba, Sudan Kusini, kati ya serikali ya mpito ya Sudan na makundi ya wapiganaji yakiongozwa na Sudan Revolutionary Front, ni hatua muhimu katika historia ya Darfur.

Alisema kuwa makubaliano kuhusu mkataba huo yataleta matumaini ya kupatikana kwa amani na utulivu katika eneo hilo.

Lacroix alipongeza pande husika kwa kujitolea kufuata mkondo wa amani pamoja na Sudan Kusini kwa wajibu wake muhimu kama mpatanishi katika mchakato huo.

“Tunapokutana hapa leo, inasalia wiki moja tu kabla ya kufanyika kwa sherehe ya kutiwa saini kwa mkataba huo, na mwanzo wa enzi mpya kwa wakazi wa Darfur,” akasema katika hotuba yake.

Hata hivyo, kazi nyingi ingali inapasa kufanywa kuhakikisha kuwa nia njema iliyoonyeshwa wakati wa mchakato wa mazungumzo inaleta mabadiliko ya kudumu katika eneo la Darfur.

Ingawa harakati hizo zimefanyika, wadau wengine wakuu kama vile kundi la Sudan Liberation Army linaloongozwa na Abdul Wahidi, bado halijajiunga katika mchakato huo.

Makubaliano hayo yangali katika hali ya stakabadhi mbalimbali na bado hayajawekwa pamoja ili kuunda stakabadhi moja itakayosheheni mustakabali wa Sudan.

Vile vile, visa vya mapigano na maandamano katika sehemu kadha za Darfur ni ishara kwamba bado kuna wasiwasi kuhusu maamuzi yanayofanywa na serikali za Sudan na Sudan Kusini.

“Kwa hivyo, jamii ya kimataifa sharti ijizatiti kuwaleta wadau wote katika mchakato huo na iimarishe juhudi za kuzuia kurejelewa kwa mapigano makubwa,” akasema Lacroix.

“Vile vile, awamu ya utekelezaji itakuwa muhimu na ile awamu ya utayarishaji wa makubaliano yenyewe. Hii itajumuisha uundaji wa kikosi cha walinda usalama chenye wanachama 12,000 ndani ya siku 90 baada ya kutiwa saini kwa mkataba huo,” alisema.

Aliendelea, “Kikosi hicho kitajumuisha wanajeshi 6,000 kutoka serikali ya Sudan na wengine 6,000 kutoka makundi ya wapiganaji. Hii ni sehemu ya mipango ya usalama katika eneo la Darfur.”

“Huku wanajeshi wakiandaliwa na rasilimali zinaletwa pamoja kupiga jeki utekelezaji wa mkataba huo, ni muhimu kuhakikisha kuwa jamii za Darfur zinaa hidi kumiliki mkataba huo na zishirikishwe katika mchakato wa utekelezaji,” akaongeza.