Makala

Unachoweza kufanya ili upone majeraha haraka

June 26th, 2020 1 min read

Na MARGARET MAINA

[email protected]

HAKUNA mtu mwenye akili razini anayependa kupata majeraha au kuchelewa kupona majeraha.

Kwa kuwa uhai na uzima wetu haupo mikononi mwetu, ni vyema tukafahamu kuwa kuna wakati tunaweza tukaumia bila ya kutarajia.

Kuna mambo unayoweza fanya ili kuharakisha kupona majeraha.

Kula vizuri

Lishe bora ni muhimu wakati wote, lakini ni muhimu zaidi mara unapokuwa na majeraha. Ili uweze kupona majeraha mapema, unahitaji ule matunda na vyakula vyenye protini, vitamini C, B12 pamoja na madini ya chuma kwa wingi.

Vyakula na matunda hayo ni kama vile machungwa, mapapai, mayai, maziwa, samaki, maharage, na kadhalika.

Kwa kula vyakula hivi, mwili utaweza kutibu majeraha kwa haraka zaidi.

Pumzika vya kutosha

Kupumzika ni njia ya kuupa mwili nafasi ya kujijenga na kujitibu wakati wa majeraha. Kutokana na mtindo wa maisha au changamoto za kiuchumi, baadhi ya watu hawapati muda wa kupumzika wapatapo majeraha. Utamkuta mtu akiendelea na shughuli zake huku akiwa na plasta au bendeji bila hata kujali.

Ili uweze kupona mapema, unahitaji kuupumzisha mwili kwa kiasi cha kutosha ili upone vyema.

Fuata maelekezo

Kutokana na majeraha uliyoyapata daktari anaweza akakukataza usile chakula hiki na kile au usifanye kitu fulani.

Watu wengi hukatazwa vitu kama vile pombe au kazi ngumu mara wapatapo majeraha.Ni lazima ufuate ushauri wa daktari ikiwa unataka kupona mapema.

Kunywa maji mengi

Maji huchukua takriban asilimia 70 ya mwili wa binadamu. Kunywa maji mengi uwapo na majeraha kutakuwezesha kupona majera hayo mapema.

Maji huboresha kingamwili, huboresha misuli pamoja na viungio (joints) mbalimbali hivyo kukuwezesha kupona majeraha mapema.

Kwa hakika lishe bora ni tiba ya maradhi karibu yote.