MakalaMichezo

UNAI EMERY: Historia ya kocha huyu itamsaidia kuifufua Arsenal?

May 26th, 2018 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

UTEUZI wa Unai Emery kuchukua wadhifa wa kocha mkuu wa Arsenal kutoka kwa Arsene Wenger umezuzua mashabiki wengi na pia kukera baadhi yao.

Je, huyu Unai Emery Etxegoien ni nani na mafanikio yake ni yepi?

Emery, ambaye atavuna Sh812.2 milioni kila mwaka (Sh270.7 milioni chini ya mshahara Arsene Wenger alikuwa akipata), alizaliwa Novemba 3 mwaka 1971.

Kama mchezaji, hana cha kujivunia. Hakuwahi kushinda taji. Alikuwa kiungo wa pembeni kushoto. Alistaafu kuwa mchezaji akiwa na umri wa miaka 32 baada ya kusakata soka yake katika Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uhispania. Aliwahi kuchezea Real Sociedad mechi tano katika Ligi Kuu msimu 1995-1996.

Emery alianza kazi ya ukufunzi mwaka 2005 akinoa Lorca na kisha Almeria alizozisaidia kuingia Ligi ya Daraja ya Pili na Ligi Kuu mtawalia kwa mara yao ya kwanza kabisa.

Alinyakuliwa na Valencia kwa kandarasi ya miaka minne na kuiongoza kumaliza Ligi Kuu katika nafasi ya tatu mara tatu katika misimu minne kati ya mwaka 2008 na 2012.

Emery alijiunga na Spartak Moscow nchini Urusi mnamo Mei 13 mwaka 2012, lakini akaangukiwa na shoka Novemba 25, 2012 kutokana na msururu wa matokeo duni.

Alitua katika klabu ya Sevilla Januari 14 mwaka 2013. Alionja taji lake la kwanza mwaka uliofuata vijana wake walipotikisa katika Ligi ya Uropa kabla ya kuhifadhi ubingwa mwaka 2015 na tena 2016.

Alinyakuliwa na mabwanyenye Paris Saint-Germain mnamo Juni 28 mwaka 2016 kwa kandarasi ya miaka miwili. Hapa alishinda mataji matatu katika msimu wake wa kwanza baada ya vijana wake kutikisa katika Kombe la Ufaransa, Ligi Kuu na shindano linalokutanisha washindi wa Kombe la Ufaransa na Ligi Kuu.

Msimu wake wa pili ulikuwa bora zaidi. Aliongoza PSG kufagia mataji manne – Ligi Kuu, Kombe la Ufaransa, League Cup na shindano kati ya washindi wa Kombe la Ufaransa na Ligi Kuu.

Aligura PSG mwisho wa kandarasi yake baada ya msimu 2017-2018 kukamilika na kuthibitishwa kocha mkuu wa Arsenal hapo Mei 23, 2018.

Emery anatoka familia ya wanasoka (babake Juan na babu yake Antonio walikuwa makipa naye mjombake Roman alikuwa kiungo). Alifunga pingu za maisha na Luisa Fernandez mwaka 1998. Wamejaliwa mtoto mmoja wa kiume, Lander, ambaye alizaliwa Machi 29, 2003.

Mashabiki wa Arsenal wanasuburi kwa hamu kubwa kuona kazi ya Emery, ambaye mtihani wake wa kwanza uwanjani utakuwa dhidi ya Atletico Madrid na PSG katika Kombe la Emirates. Emery anapenda kutumia mfumo wa kucheza 4-2-3-1 na 4-3-3.

Wenger, ambaye alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu na saba ya Kombe la FA katika miaka 22 alikuwa Arsenal, alipenda 4-4-2, ingawa alikuwa akibadilishabadilisha hadi 3-4-2-1, 3-4-3, 4-3-1-2 na 4-2-3-1.