Michezo

Unai kugeuza Ozil injini dhidi ya Chelsea

May 23rd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

KOCHA wa Arsenal, Unai Emery amesisitiza kwamba Mesut Ozil atakuwa tegemeo kubwa kwenye fainali ya Europa League dhidi ya Chelsea jijini Baku nchini Azerbaijan, Jumatano ijayo.

Ozil amerejelea fomu yake bora chini ya Unai Emery baada ya kusuasua kwa muda mrefu hapo awali kwa kutozoea mbinu za kocha huyo raia wa Uhispania.

“Uwepo wa Ozil utatufaa sana, kutokana na ujuzi wake wa miaka mingi kwenye mechi za bara Ulaya,” kocha huyo alisema kupitia kwa mtandao wa arsenal.com.

“Tunaandaa wachezaji wetu wote wawe tayari kwa mechi hii kubwa. Ozil ni miongoni mwao na anaendelea vizuri na mazoezi. Tutamhitaji.”

Arsenal itakuwa bila Henrikh Mkhitaryan ambaye ameondolewa kikosini kwa sababu za kiusalama.

Wakati huo huo, mshambuliaji Alex Iwobi amesema anatarajia ndoto yake ya kutwaa mataji akiwa na The Gunners kutimia watakapokutana na Chelsea kwenye fainali ya Europa League juma lijalo.

Iwobi mwenye umri wa miaka 23 amekuwa na Arsenal tangu 2004, na fainali ijayo itakuwa yake ya kwanza ya kiwango cha bara tangu washindwe na Barcelona katika fainali ya Klabu Bingwa Ulaya mnamo 2006.

“Kuwa hapa na kupata nafasi ya kucheza fainali ya kiwango hiki ni fursa kubwa ya kujivunia maishani, alisema Iwobi akizungumza kuhusu fainali hiyo itakayofanyika Mei 29.

“Nilikuwa na matumaini makubwa ya kutwaa mataji nikiwa Arsenal hata nilipokuwa na umri mdogo. Sikujua nitafika nao katika kiwango hiki cha juu. Taji lolote kwetu ni muhimu, daima tutapigana vikali kila tunapopata fursa ya kuwania ubingwa, na Europa League ni fainali kubwa ambayo tungependa kushinda,” aliongeza raia huyo wa Nigeria.

Taji la FA

Akiwa na Arsenal, Iwobi ameisaidia kutwaa taji la FA Cup na mengine mawili ya League Cup maarufu kama Carabao Cup.

Akizungumza kuhusu fainali hiyo, kipa Petr Cech anayehusishwa na mpango wa kujiunga na Chelsea kama mkufunzi wa makipa amesisitiza kuwa kwa sasa mawazo yake yanalenga kuisaidia Arsenal kutwaa ubingwa.

Waandishi walimuuliza swali hilo kufuatia ripoti zilizoenea kwamba Chelsea imemuitia kazi ya kuwa mkuu wa idara ya kuwafundisha makipa baada ya fainali ya Europa kumalizika.

Kupitia kwa mtandao wa Twitter, Cech alisema, “Licha ya habari zinazoenea kote, tayari nilikuwa nimetangaza kwamba nitafanya uamuzi wangu baada ya kustaafu kazi ya kulinda lango. Kwa sasa najipanga kwa fainali kama mchezaji wa Arsenal.”

Cech, ambaye alifikisha umri wa miaka 37 Jumatatu, alijiunga na Chelsea mnamo 2004 akitokea Rennes ya Ufaransa na kuisaidia kutwaa mataji mbalimbali, yakiwemo manne ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo 2012 kabla ya kujiunga na Arsenal mnamo 2015.