Makala

Unavyoweza kutahadhari usipatwe na janga mafuriko yanapotokea

April 27th, 2024 1 min read

NA LABAAN SHABAAN

HUKU mvua kubwa ikiendelea kuponda sehemu nyingi nchini, Shirika la kutoa misaada la Red Cross limeorodhesha ushauri kwa Wakenya kuepuka madhara.

Maeneo yanayoathiriwa na mafuriko ni ukanda wa Ziwa Victoria, Bonde la Ufa, Kusini Mashariki, Pwani, Kaskazini Mashariki na Nairobi.

Sambamba na serikali, Red Cross inashauri Wakenya wanaoishi nyanda za chini kuhamia maeneo ya juu ili waepuke kusombwa na maji endapo mafuriko yatatokea.

Wakati panapotokea mafuriko hadi ndani ya makazi, shirika hili limeelekeza waathiriwa kuzima umeme kuepuka hatari zaidi.

“Nyumba ikifurika, zima stima kutumia swichi kuu,” iliandika Red Cross kwenye mtandao wa kijamii wa X.

Jingine ambalo Wakenya wametahadharishwa kwalo ni kutembea kwenye maji yanayotiririka ardhini.

“Hata maji ya kina cha inchi sita kitakuangusha!” onyo lilitolewa kwa wanaojasiria kutembea majini.

“Futi moja ya maji yanayosonga pia yanaweza kusomba gari,” madereva walitahadharishwa.

Kisha shirika hili likaongeza: “Epuka kuegesha, kuendesha magari ama kujishughulisha na mambo nje wakati wa mafuriko.”

Vile vile Red Cross inawataka Wakenya kupima kina cha maji kwa kijiti kabla ya kupita maeneo yaliyofurika.

Mvua inayoendelea kunyesha imeharibu miundomsingi ya usafiri na hili likizingatiwa, waendeshaji magari wamekanywa wasipite kwenye madaraja yaliyoathiriwa na mafuriko.

Kadhalika, milingoti ya umeme imesombwa na kuangushwa na mafuriko yanayoendelea.

Kwa hivyo, wakazi wametahadharishwa wasikae chini ya nyaya za umeme.

Isitoshe, Red Cross imewashauri wasikaribie maeneo yaliyo na maji kama vikingi vya stima vimeanguka.