Makala

Unaweza kukataa mali uliyoachiwa kwa roho safi

Na BENSON MATHEKA August 30th, 2024 2 min read

MTU anaweza kukataa mali anayoachiwa katika wosia akitaka kufanya hivyo.

Katika kisa kimoja, Rita Field- Marsham  binti ya aliyekuwa waziri Nicholas Biwott aliahiri kuondolewa katika orodha ya waliotajwa kunufaika na mali ya babake.

Alifanya hivi kwa kuandikia mahakama barua akiomba aondolewe miongoni mwa waliotajwa katika wosia wa babake kama warithi wa mali ya mabilioni.

Kupitia barua hiyo, aliondoa haki yake ya kudai urithi wa mali ambayo alikuwa ameachiwa na babake.

Ikiwa kuna mali unayomiliki pamoja na mtu mwingine na afariki dunia, mali hiyo inabaki kuwa yako.

Mali hii inaweza kuwa inayohamishika kama gari, hisa na pesa au isiyohamishika kama mashamba na nyumba.

Mali huwa inabaki kuwa ya aliye hai hata kama aliyekufa alikuwa ameacha wosia.

Kwa hivyo, inachukuliwa kuwa, mmiliki halali ni yule anayebaki hai kabla ya masuala ya wosia wa anayefariki kuibuka.

 Hata hivyo, iwapo anayefariki alikuwa ameacha maagizo benkini kuhusu mali aliyomiliki pamoja na anayebaki hai, yanaweza kuzingatiwa.

Maelezo ya benki huwa ni muhimu sana pale akaunti inamilikiwa na watu wawili kwa kuwa yanaweza kutoa mwelekeo wa anayefaa kunufaika na sehemu ya anayefariki dunia.

Iwapo anayefariki anaacha wosia akipatia baadhi ya warithi wake mali nyingi kuliko wengine, korti haiwezi  kubatilisha wosia wake.

Inafaa kukumbukwa kuwa, wosia huandikwa na mtu kwa hiari yake akiwa na akili timamu na buheri wa afya kumaanisha kuwa anajua anachofanya.

Sehemu ya tano ya sheria ya urithi ya Kenya inapatia kila mtu mzima, mwenye akili timamu, uhuru wa kugawa mali yake anavyotaka.

Hii inahusu uhuru wa kugawa mali hiyo kwa kiasi anachotaka kwa yeyote anayetaka.

Mahakama inaweza tu kuingilia uhuru huu iwapo anayeacha wosia anakosa kuachia watoto wake au watu waliomtegemea mali ya kutosha.

Na hata inapofanya hivi, mahakama haiwezi kufuta au kubatilisha wosia lakini inaweza kutoa agizo la kupatia anayeachwa nje ya wosia sehemu ya mali au kuongeza kiasi kwa mtu aliyekuwa akitegemea marehemu aweze kukidhi mahitaji yake.

Ni muhimu kukumbuka kuwa ni lazima mtu anayedai sehemu ya mali ya mwendazake athibitishie korti kwamba alikuwa akimtegemea marehemu alipokuwa hai na hana uwezo wa kukidhi mahitaji yake  kwa kuachwa nje ya wosia au kiasi alichoachiwa hakiwezi kukidhi mahitaji hayo.