Makala

Unilever Tea Kenya yasisitiza kuweka ua wa stima kuzima wezi

December 14th, 2018 2 min read

Na ANITA CHEPKOECH

KAMPUNI ya Unilever Tea Kenya imetetea uamuzi wake wa kuweka ua wa kulinda mashamba yake pana ya majani chai eneo la South Rift, ikisema ni mbiu mwafaka ya kuzima wezi wanaoiba majani chai yake na kuwasababishia hasara kuu.

Mkurugenzi wa Masuala ya Biashara katika kampuni hiyo, Bw Joseph Sunday aliambia Taifa Leo kuwa wamekuwa wakishuhudia majambazi waliojihami wakivamia mashamba yao na kuvuna majani chai na kuwatishia wafanyakazi wake.

Hii ni baada ya Gavana wa Kericho Paul Chepkwony na mbunge wa Belgut Nelson Koech kupinga mpango wa kuweka ua wa umeme wa Sh70 milioni, wakisema hatua hiyo itawatenga wakazi ambao wametangamana vyema na kampuni hiyo kwa karne nzima.

Bw Sunday alisisitiza kuwa kampuni hiyo ililazimika kuchukua hatua hiyo ili kuwahakikishia wafanyakazi, mali ya kampuni na uchumi wa majani chai usalama.

“Sisi na washikadau wa hapa tumeng’amua ongezeko la wizi, dhuluma na uharibifu wa mali. Mtingo huu umezua kupungua kwa mapato,” akasema.

Ingawa alidinda kufichua kiwango cha pesa kampuni hiyo imepoteza kutokana na mtindo huo wa mwaka mzima, inaaminika mamilioni yameporwa na wezi.

Gavana Chepkwony alisem akuwa Unilever ilifaa kushauriana na ofisi yake mwanzo kwa kuwa ardhi hiyo inamilikiwa na kaunti yake lakini inashikiliwa na Tume ya Ardhi Nchini.

“Mpango wa Unilever wa kuweka ua wa stima kuzunguka shamba lake unalenga kuwatenga wakazi. Utawafungia nje wakazi wa Kericho kutangamana na kampuni hii,” akasema Prof Chepkwony.

Kampuni hiyo kutoka Uingereza ni majawapo ya zile ambazo hadi 2010 zilikuwa zinamiliki shamba la ekari 800 eneo la South Rift katika makubaliano ya ukodishaji wa miaka 999.

Lakini miaka hiyo ilipunguzwa hadi 99, baada ya Kenya kupata katiba mpya, kumaanisha umiliki huo sasa utaisha mwaka 2109 ambapo serikali itatwaa ardhi hiyo.

Gavana huyo ambaye amekuwa akiandaa kesi dhidi ya serikali ya Uingereza kwa kuwatimua wakazi ili kuwekeza kwa mashamba ya kikoloni ya majani chai miaka ya 1900, amesema tayari ametuma barua kwa makao makuu ya kampuni ya Unilever Tea Company nchini Uingereza kupinga suala hilo.

Naye Bw Koech alisema hatua hiyo itawazuia wakazi kupata huduma za kijamii kama elimu, maji na barabara ambazo zinapitia ndani ya shamba hilo.

“Tunaiomba Unilever kusimamisha wazo hili. Iwapo watasisitiza, nitawachochea wakazi wa Belgut kubomoa majengo yote,” akatisha mbunge huyo.

Hata hivyo, Bw Sunday alisema uamuzi wa kampuni yake hauwezi kubatilishwa.

“Ua huo wa stima utajengwa katika shamba nzima la Unilever, ili kulinda uwekezaji wetu na kuweka viingilio kupitia kwa barabara za shambani kuhakikisha uhuru wa kutembea umeendelea,” akasema.