Habari Mseto

Unilever yajikakamua kupenya kwa soko la dawa ya meno

March 21st, 2019 1 min read

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya Unilever imepunguza bei ya dawa ya meno ya Pepsodent kwa zaidi ya nusu kwa lengo la kukuza soko lake nchini.

Kampuni hiyo ilipunguza bei ya gramu 150 za dawa hiyo hadi Sh99 kutoka Sh199 ili kupata wateja zaidi kutokana na ushindani mkali sokoni.

Kwa muda wa miaka mitano, kumekuwa na ongezeko la aina tofauti za dawa za meno. Zaidi ya Pepsodent, Unilever inamiliki Close-Up.

Colgate-Palmolive huuza Colgate ilhali GlaxoSmithKline Kenya hutengeneza Aquafresh.

Gramu 150 za Colgate Herbal huuzwa kwa Sh220 ilhali Close-Up ya gramu 125 ambayo huuzwa kwa Sh220 na gramu 110 za White Dent huuzwa kwa Sh160.

“Ili kusaidia kukuza azma ya kutumia dawa hii na kuwa washindani, kampuni zinatakiwa kuwa bunifu kwa mfano kutumia viungo asili na dawa za kienyeji na kufanya kampeni mara kwa mara,” ilisema kampuni ya utafiti Euromonitor kuhusiana na uchanganuzi wa soko la Kenya.

Unilever Jumatano ilisema inalenga kutoa bidhaa ambazo zitaimarisha afya ya meno kwa bei ambayo wengi wanaweza kumudu.

“Pia tumetoa sampuli za thamani ya Sh25milioni katika shule 225 Nairobi,” alisema mkurugenzi wa maslahi ya kibinafsi Afrika Mashariki Pawan Marella.