Makala

UNYAKUZI WA ARDHI: Mayatima waililia serikali ya Kiambu iwasaidie kumiliki ardhi

January 23rd, 2019 3 min read

Na CHARLES WASONGA

KWA muda wa miaka miwili sasa vijana wawili mayatima kutoka eneo bunge la Kikuyu, kaunti ya Kiambu wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi baada ya watu fulani kutisha kunyakua ploti ambako tangu utotoni walijua ni mali ya marehemu nyanya yao, Esther Warugu Wakaba.

Na juhudi za wawili hao Samuel Ndung’u Wakaba, 26 (pichani) na David Ngugi Wakaba (29) za kutaka kupata hatimiliki ya ploti hiyo nambari 42 iliyoko mjini Kikuyu zimehujumiwa kila mara na maafisa wa serikali ya Kaunti ya Kiambu.

Wanasema hata baada ya Tume ya Kitaifa ya Ardhi (NLC) kutoa amri ya kuzuia unyakuzi wa kipande hicho cha ardhi cha nusu ya robo ekari (1/8) na kuitaka serikali ya kaunti ya Kiambu ithibitishe kuwa ardhi hiyo iliyoko Kikuyu Mjini ni yao, hawajapata msaada wowote.

“Baada ya unyakuzi huo kusimamishwa, tume ya NLC ilituambia tuende kwa serikali ya kaunti ya Kiambu ili tuandikiwe barua ya kuidhinisha kuwa ardhi hiyo iko katika kituo cha kibiashara cha Kikuyu Mjini. Vile vile, tume hiyo ilitaka kaunti ya Kiambu ithibitishe kwa nyanya yetu ndiye alikuwa akiishi hapo huku akiilipia kodi hadi Machi 1, 2012, lakini juhudi zetu hazijafanikiwa hadi sasa,” akasema Ndung’u.

“Na mwaka 2018 dadake nyanya yetu Jane Wambui alifuatilia suala hilo hadi kwa afisi ya Gavana Ferdinard Waititu. Gavana huyo aliguzwa na kilio chetu na akaamuru msimamizi wa kaunti ndogo ya Kikuyu Bw Kingori atuandikie barua hiyo kuthibitisha uhalali wetu wa kuendelea kuitumia ploti hiyo kama watu wa familia ya marehemu nyanya yetu lakini hajafanya hivyo mpaka leo,” akaelezea Taifa Leo kwa machungu.

Stakabadhi kutoka kwa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) zinaonyesha kuwa Esther Ruguru Wakaba alilipa kodi ya ardhi hiyo mara ya mwisho mnamo Januari 1, 2012. Nakala ya risiti hiyo ya malipo inaonyesha kuwa KRA ilipokea Sh250 kutoka kwa Bi Wakaba kama kodi ya mwaka huo wa 2012.

Hii ni ithibati, kama wanavyodai wajukuu hao, kwamba nyanya yao alikuwa akilipia ardhi hiyo kodi hadi hadi alipofariki mnamo mwezi Machi mwaka huo.

Hata hivyo, kizungumkuti cha sasa kinachowakabiliwa Ndung’u na Ngugi kinatokana na hali kwamba nyanya yao aliaga dunia kabla ya kupata hati miliki ya kipande hicho cha ardhi licha ya kuilipia kodi kwa zaidi ya miaka saba.

Na hii, wanasema, ndio maana mnamo Februari 15, 2017 watu fulani waliodaiwa kuwa maafisa wa chama cha KANU tawi la Kikuyu waliwapa vijana hao, ambao wamekuwa wakiishi katika nyumba ya mabati ya nyanya hapo, notisi ya siku 14 waondoke.

“Na baada ya kupata ilani hii tuliomba usaidizi kutoka kwa dadake nyanya yetu Bi Jane Wambui aliyekodi huduma za wakili Tim Okwaro ambaye aliwaandikia wanyakuzi hao na wakasimamisha ilani ya kutufurusha,” akaeleza Ndung’u.

David Ngugi Wakaba. Picha/ Charles Wasonga

“Ndipo mnamo Septemba, 2017 sisi kama familia tuliandikia NLC tukitaka usaidizi ili tupate hatimiliki ya ploti hii. Lakini tume hiyo iliturejesha kwa Serikali ya Kaunti ya Kiambu ili ithibitishe kama sisi ni warithi halali wa ploti hiyo ambayo nyanya yetu aligawiwa mapema miaka ya 1990s,” akaeleza.

Kulingana na barua ya NLC iliyotiwa saini na Muthoni Ngaruthi kwa niaba ya Mwenyekiti Mohammed Swazuri, na kutumwa kwa Katibu wa Kaunti ya Kiambu mnamo Julai 18, 2018, tume hiyo inaomba kurejelea rekodi zake na kuipa mapendekezo kuhusu umiliki wa ploti hiyo.

“Familia ya Esther Ruguru Wakaba (marehemu) imewasilisha madai kuhusu ploti nambari 42 iliyoko katika kituo cha kibiashara cha Kikuyu, kaunti ya Kiambu. Rekodi zilizoko zinaonyesha kuwa ardhi hiyo ni ya umma na inapatikana Kikuyu mjini. Tafadhali kagua rekodi zenu kuhusu hali yake na uniwasilishie mapendekezo yenu,” NLC ikasema kwenye barua hiyo ambayo ilipokewa na serikali ya kaunti ya Kiambu mnamo Julai 30, 2018.

Na siku hiyo hiyo,Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Ardhi, Nyumba na Mpango wa Miji Isaac Kinuthia alimwandikia barua Msimamizi wa kaunti ndogo ya Kikuyu akimtaka kuwasilisha maelezo kuhusu kuhusu kipande hicho cha ardhi, ploti nambari 42.

Lakini hadi wakati huu, msimamizi huyo ambaye anafahamika kwa jina moja la Bw Keng’ori, hajajibu barua hiyo kwa kutoa maelezo alivyoagizwa na Bw Kinuthia.

Hii ndio maana familia ya marehemu Wakaba sasa imeingiwa na wasiwasi kwamba huenda afisa huyo anashirikiana na wale ambao wanalenga kuwapokonya umiliki wa kipande hicho cha ardhi.

“Hatua ya msimamizi wa kaunti ndogo ya Kikuyu kunyamazi suala hili imeibua hofu kwa wajukuu wa dadangu kwamba huenda yeye pia ni mshirika katika njama ya kuwapokonya ploti hiyo ambayo wao ni warithi wake halali” akasema Mama Wambui ambaye ni dadake marehemu Mama Wakaba.

“Sasa mayatima hawa wanaomba msaada kutoka viongozi wa kaunti ya Kiambu kuanzia Gavana Waititu, Mbunge Kimani Ichung’wa hadi Diwani wa wadi ya Kikuyu Mjini Bw Henry Kagiri ili waweze kupata barua ya kuidhinisha kuwa nyanya yao ndiye mmiliki halali wa ploti hiyo. Barua hiyo ndiyo itawawezesha kupata hatimiliki ya ploti hiyo,” anasema akaongeza.

Ndung’u na Ngugi wanasema kuwa baba yao Paul Wakaba Ruguru alifariki ambaye ndiye alikuwa kijana mkubwa wa nyanya yao alifariki mnamo 1993. Kisha miaka miwili baadaye, mnamo 1995 mama yao, Bi Phylis Nyakeo vile vile akafariki.

Walibaki wakiishi katika nyumba ya nyanya yao kwenye ploti hiyo hadi walipoanzia kutishiwa na wanyakuzi hao.