Unyama magaidi wakilipua ambulensi ya mjamzito

Unyama magaidi wakilipua ambulensi ya mjamzito

Na MARY WAMBUI

MTU mmoja alifariki baada ya magaidi kushambulia ambulensi ya Serikali ya Kaunti ya Mandera usiku wa kuamkia Jumatano.

Kulingana na polisi, ambulensi hiyo aina ya Toyota Land Cruiser ilikuwa ikimsafirisha mwanamke mjamzito kutoka hospitali ya Kotulo kuelekea Elwak ilipovamiwa katika eneo la Dabacity na watu wanaoaminika kuwa wanamgambo wa Al-Shabaab.

Washambuliaji hao walimpiga risasi mume wa mwanamke huyo na kumuua papo hapo kabla ya kulipua gari hilo kwa kutumia kilipuzi.

Walitoweka punde baada ya tukio hilo.Wengine waliokuwamo ni dereva wa ambulensi hiyo, mamake mwanamke huyo na nesi aliyekuwa akiandamana na mgonjwa.

Mkuu wa Polisi eneo la Kaskazini Mashariki Rono Bunei alisema mwanamke huyo yumo hospitalini lakini katika hali mahututi.

Wakati huo huo, polisi katika eneo la Mandera wanamzuilia mshiriki wa Al Shabaab aliyekamatwa na polisi waliokuwa wakipiga doria katika eneo la Banisa Jumatano.

Jijini Nairobi, washukiwa wawili wa kigaidi walikamatwa na polisi mnamo Jumanne saa kumi na moja jioni baada ya raia kuripoti kuwaona watu wa kutiliwa shaka katika Soko la Mbuzi, Kiamaiko.

Raia huyo wa Yemen na Mkenya waliwekwa katika kizuizi cha polisi wakisubiri uchunguzi kufanywa.

 

You can share this post!

Usiwatambue Wapemba kwa vilemba pekee, wana sifa nyingine...

2020: Wizi serikalini, migomo na ukosefu wa ajira corona...