HabariMakala

UNYAMA: Mke kutoka kuzimu alivyompa mumewe upofu daima milele

February 4th, 2019 3 min read

Na CECIL ODONGO

KILA mwaka Kenya inapowakumbuka wahanga wa shambulizi la kigaidi la Westgate lililotokea Septemba 21, 2013, uchungu, ukiwa na masikitiko humvaa Dan Matakaya, mzaliwa wa kijiji cha Shakunga, eneobunge la Shinyalu, Kaunti ya Kakamega.

Bw Matakaya ambaye ni afisa wa polisi wa hadhi ya konstebo katika kituo cha polisi cha Industrial Area, Nairobi, milele daima hatawahi kusahau siku hiyo ya mauti si kwa Wakenya hao tu bali hata kwake yeye mwenyewe.

Kwake, tukio la kusikitisha alilowahi kukumbana nalo mikononi mwa aliyekuwa mkewe limemfanya kipofu ingawa alizaliwa mzima wa afya tena bila kasoro au tatizo lolote la kimaumbile.

Kama ada, Bw Matakaya ambaye wakati huo alikuwa afisa wa polisi katika kituo cha polisi cha Kisii ya Kati mjini Kisii siku hiyo alirejea katika makazi yake kituoni humo baada ya kuwajibikia majukumu yake ya kikazi usiku kucha.

Akiwa amevamiwa na uchovu na usingizi mwingi, afisa huyo aliingia chumbani saa 11 asubuhi na kujilaza kitandani ili kupumzika huku aliyekuwa mkewe ambaye aliomba jina lake lisitajwe kwa sababu za kiusalama na kesi iliyoko mahakamani, akiwa anajishughulisha na usafi wa nyumba yao.

Wawili hao walikuwa wamevurugana siku iliyotangulia baada ya Bw Matakaya kumzima mkewe aliyefaa kusafiri kwao siku hiyo kutobeba nguo za marehemu mtoto wao aliyefariki miezi michache ya awali, hadi kwao.

Suala hilo siku iliyotangulia lilikuwa limezua ubishi mkali kati yao.

“Tulikuwa tumejaaliwa mtoto katika ndoa yetu changa lakini kwa masikitiko makuu akafariki miezi michache baada ya kuzaliwa kwake. Mke wangu alifaa kuenda kwao lakini sikuelewa kwa nini alitaka kupeleka nguo za mwanangu kwao. Niliwapigia simu wakwe wangu na kuwaeleza kuhusu suala hilo na wakakubaliana nami kwamba binti yao hakufaa kubeba nguo hizo ndipo nikamkataza,” Bw Mataya akasema wakati wa mahojiano katika jumba la Nation Centre, jijini Nairobi.

Akiwa amepata usingizi wa pono, mkewe, aliyekuwa na umri wa miaka 23 wakati huo na mara nyingi akionekana mnyamavu na mtulivu, alikuja kitandani akiwa amebeba kemikali ya Sulphur aliyotia ndani ya maji moto na kummwagia usoni.

“Nikiwa usingizini nilihisi maumivu makali machoni ila sikuweza kuonana hata baada ya kutapatapa kama mfa maji. Nilijizoazoa kumkabili lakini nikashindwa baada ya kukanyaga nyaya za stima alizokuwa ameunganisha kisha kuzimwagia maji sakafuni ili nichomeke,” akafafanua Bw Matakaya.

Akiwa na maumivu makali, afisa huyo ambaye pia aliwahi kudumu katika kituo cha polisi cha Etabwa mjini Embu alisimulia namna majirani walivyofika na kunusuru maisha yake baada ya kupiga ukemi akilia na kuitisha msaada.

Mkewe naye baada ya kitendo hicho aliingia mafichoni ila akaibuka baada ya siku mbili na kujiwasilisha kwa maafisa wa polisi kituoni humo ambako alizuiliwa kabla ya kufikishwa katika mahakama ya Kisii kujibu mashtaka ya nia ya kuua. Aliachiliwa kwa dhamana siku chache baadaye.

Akiwa amesononeka, Bw Matakaya alisema kwamba harakati ya kupata haki imekuwa ikijikokota sana. Hii ni kutokana na mazoea ya jaji anayeshughulikia kesi hiyo kuiaihirisha kila mara bila sababu za kuridhisha.

“Kesi imekuwa ikijikokota sana tangu mwaka wa 2013 lakini nina imani kwamba ipo siku nitapata haki,” akasema Bw Matakaya akiwa ameandamana na Wycliffe Manyengo ambaye alimwajiri kama mwelekezi wake baada ya kupofuka.

Katika hali ya kushangaza, afisa huyu anasema kwamba hana kinyongo na mkewe na amemsamehe rohoni lakini hawezi kuondoa kesi kortini maana ameshauriwa kutofanya hivyo.

Anafichua kwamba amekuwa akipokea jumbe za watu kutoka familia ya mkewe wanaosikitikia hali yake na kumwomba amsamehe ila anasisitiza kwamba hawezi kurudiana naye kamwe na wao hukutana tu wakati wa vikao vya kesi wala hawajawahi kuzungumza kwa simu tangu mwaka wa 2013.

Bw Matakaya pia alituelezea kwamba tukio hilo liliathiri sana wazazi wake John Matakaya na Bilha Matakaya ambao walichukua muda sana kukubali kwamba mwanao tegemeo amekuwa kipofu bila kosa wala hatia.

Kikazi, afisa huyo aliwashukuru sana wenzake wa kituoni kwa kumpa msaada mkubwa kila mara anapowahitaji japo alisisitiza kwamba hali yake haijamzuia kutekeleza wajibu wake kama kawaida baada ya kupokea masomo ya namna ya kuwasiliana na kuandika kutumia mashine za Braille zinazotumiwa na wasioona.

“Masomo hayo yamenisadia sana kwasababu naweza kuandika, kusoma, kupiga simu na kazi nyingine za polisi baada ya simu yangu kuwekewa teknolojia ya kisasa inayonirahisishia kuandika na kuongea. Pia maafisa wenzangu na mwelekezi wangu Bw Manyengo wamekuwa wazuri sana kwangu. Kwa kweli namshukuru Mungu na namwomba awazidishie neema,” akaongeza Bw Matakaya.

Akilenga ufanisi na kuwaokoa wanaodhulumiwa, afisa huyo yuko kwenye mchakato wa kuanzisha wakfu kwa jina Dan Shieshie utakaowanusuru waume na wake wanaopitia madhila katika ndoa zao na mambo mengine mabaya yanayotokea katika jamii.

Kulingana naye, wanaume wengi huathirika sana katika ndoa zao japo huwa hawajitokezi kusema kwa hofu ya kuchekwa au kutazamwa tofauti na jamii ambayo huwachukulia kama wakuu wa familia wasiofaa kupigwa na wake.

Hata hivyo yeye amejitolea kuwasaidia kwa kuwapa ushauri na misaada mingine akitumia hela zake.

“Jambo la kweli ni kuwa ndoa nyingi zina pandashuka na wanaoumia zaidi ni wanaume wanaosalia kimya wakiwa na hofu ya kuchekwa. Nimeweka nambari yangu wazi ili waweze kuwasiliana nami kwa sababu niko tayari kuwasaidia hata kwa fedha zangu wasije wakajiua au kufanya mambo yasiyofaa baada ya kuathiriwa kisaikolojia,” akasisitiza afisa huyo.

Ili kudhihirisha matamanio yake ya kuwapa msaada wanaoathirika ndipo yaliyomkuta yasiwapate, Bw Matakaya anasomea shahada ya Ushauri Nasaha katika Chuo Kikuu cha Mlima Kenya bewa la Nairobi.

Anatumai masomo haya yatamwezesha kushughulikia kesi zitakazowasilishwa kwa wakfu wake ama zile atapokea kupitia mawasiliano ili kuwaepusha wengi kukumbana na msiba kama wake.

Pendekezo lake kwa serikali kupitia wizara ya afya ni kwamba mauzo ya wazi ya asidi au kemikali hatari yanafaa kudhibitiwa.