Habari

Unyama wa kutisha mwanamke mgonjwa kuuawa

February 5th, 2019 2 min read

Na HILARY KIMUYU na VALENTINE OBARA

HUZUNI ilitanda Jumatatu kwa jamaa na marafiki wa Mildred Odira, ambaye alikuwa ametoweka wiki iliyopita akiwa mgonjwa, wakati mwili wake ulipopatikana katika hifadhi ya maiti ukiwa na majeraha usoni na sehemu za chini za mwili.

Wengi walibaki wakijiuliza maswali kuhusu chanzo cha kifo cha mfanyakazi huyo wa huduma za simu katika Kampuni ya Nation Media Group (NMG), ambaye alikuwa ameajiriwa kupitia shirika la Foresight kwani suruali aliyovaa ilikuwa imeraruka huku chupi ikionekana kuvuka.

Wafanyikazi wenzake na marafiki katika orofa ya tatu ya NMG waliangua kilio jana asubuhi walipopokea habari kuwa mwili mwenzao umepatikana City Mortuary, Nairobi na kuashiria alikuwa ameuawa kikatili na hali alikuwa anaugua.

Bi Odira, mama ya mtoto mwenye umri wa miaka tisa, alikuwa ametoweka Jumanne iliyopita baada ya kuchukuliwa na teksi nyumbani kwake mtaani Kariobangi South mwendo wa saa kumi usiku kupelekwa hospitalini kwa vile alikuwa anaugua.

Jana, familia yake ilitaka polisi kuchunguza kikamilifu kisa hicho waliomuua wanaswe na kushtakiwa.

Rekodi zilizo katika hifadhi ya maiti ya City, ambapo mwili wake ulipatikana jana asubuhi, zilionyesha alipelekwa huko na polisi wa trafiki wa kituo cha Kasarani mnamo Jumanne iliyopita, saa kumi na mbili na dakika 31 asubuhi na akaorodheshwa kama mtu asiyetambuliwa.

Wasimamizi katika hifadhi hiyo ya maiti walieleza kwamba polisi waliompeleka huko walisema mwili wake ulipatikana katika eneo la Mwiki.

Kabla ya kutoweka kwake, Bi Odira alikuwa amegunduliwa kuwa anaugua kisukari, shinikizo la damu na vidonda vya tumbo.

Mhudumu wa teksi aliyeonekana naye mara ya mwisho alikamatwa na polisi Jumamosi. Walinzi katika mtaa wa Kariobangi South ndio walikuwa wamemwita dereva huyo kumpeleka Bi Odira hospitalini.

Familia ya marehemu ilipomuuliza dereva huyo Ijumaa kabla akamatwe kuhusu alikompeleka Bi Odira, alidai alimpeleka katika Hospitali ya Ruaraka Uhai Neema iliyo mkabala wa uwanja wa Kasarani, akaondoka baada ya dakika 20 pekee na kumwacha mgonjwa huko.

Lakini rekodi za hospitali zilionyesha dereva huyo aliingia kwenye lango la hospitali saa kumi unusu usiku na kuondoka saa kumi na moja na dakika 57, ambao ni muda wenye tofauti kubwa ikilinganishwa na dakika 20 alizoarifu familia yake.

Katika hospitali hiyo, wasimamizi walisema hapakuwa na rekodi yoyote iliyoonyesha Bi Odira alipokewa hospitalini humo. Kamera za CCTV pia zilionyesha teksi husika ikiingia na kuondoka bila kumwacha mtu yeyote hapo ndani.

Wafanyakazi wenzake walikuwa wamesema alikuwa kazini mara ya mwisho Alhamisi, Januari 24 ambapo aliomba ruhusa kwenda hospitalini kwani shinikizo la damu lilimzidi. Alihitajika kurudi tena hospitalini Jumatatu.

Dadake, Bi Maureen Anyango alieleza kuwa alimwona mara ya mwisho Jumapili wiki hiyo wakati alipoenda kumpikia pamoja na mwanawe.

Ni wakati mtoto wake alipoenda nyumbani kwa shangazi yake Jumanne asubuhi ndipo familia iligundua kulikuwa na tatizo.

“Tulimuuliza kwa nini hakuwa shuleni akasema mamake alitoka mapema sana ndipo tukaanza kuulizia alikoenda,” akasema Bi Anyango, ambaye alijaribu kumpigia dadake simu lakini ikawa imezimwa.

Kifo cha Bi Odira kimetokea wakati ambapo visa vya mauaji vinazidi kuripotiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.