Unywaji pombe unachangia matatizo ya akili – Nacada

Unywaji pombe unachangia matatizo ya akili – Nacada

Na WINNIE ATIENO

WAKENYA wameshauriwa wasinywe pombe na kutumia mihadarati ambayo imetajwa kuchangia maradhi ya akili nchini.

Prof Mabel Imbuga, ambaye ni mwenyekiti wa bodi ya Mamlaka la Kitaifa ya Kupambana na Mihadarati Nchini (Nacada) aliwaonya Wakenya dhidi ya unywaji wa pombe na matumizi ya mihadarati ambayo yanachangia maradhi ya akili.

Prof Imbuga alisema Wakenya wanafaa kuangalia afya yao.

“Wakenya wanafaa kususia pombe na utumizi wa mihadarati ambayo inachangia maradhi ya akili. Waachane na pombe na mihadarati kabisa, ni hatari. Kama unashindwa kupambana na uraibu huo unaweza kupata matibabu katika vituo vya Nacada,” alisema Prof Imbuga.

Akiongea huko Mombasa kwenye mkutano wa Nacada, Prof Imbuga alisema Nacada itahakikisha kuna vituo vya kurekebishia tabia na kumpambana na uraibu sugu wa mihadarati katika kila kaunti.

Naye afisa mkuu wa Nacada Bw Victor Okioma alisema serikali itapambana na ulanguzi wa mihadarati nchini.Alisema visa vya matitizo ya akili vimeongezeka nchini kufuatia uraibu sugu wa mihadarati hasa sehemu za pwani.

“Sehemu ya Pwani imeathirika pakubwa na janga la mihadarati ambayo imechangia watu kupatia maradhi ya akili hasa vijana,” alisema Bw Okiama.

Aliongeza kuwa Rais Uhuru Kenyatta aliamrisha kupanuliwa kwa kituo cha wagonjwa wa akili cha Mathari jijini Nairobi kukabiliana na wagongwa wengi wanaokabiliwa na hali hiyo.

Mshirikishi wa eneo la Pwani John Elungata aliwataka wazazi kulinda watoto wao wasiingie kwenye uraibu huo.

You can share this post!

JAMVI: Huyu atakayembwaga Ruto Mlimani ni nani?

Matumaini tele kiwanda cha sukari kianze kunguruma tena