Habari Mseto

Uokoaji waendelea kunusuru waliokwama jengoni Tassia

December 9th, 2019 1 min read

NA COLLINS OMULO

MAJONZI, masikitiko na vilio Jumapili vilitanda kwa siku ya pili wakati familia kadhaa zilipokuwa zikisubiri wapendwa wao waokolewe kwenye vifusi vya jengo lililoporomoka katika mtaa wa Tassia, Nairobi Ijumaa iliyopita.

Ukiwa huo unaendelea huku Naibu Kamishina wa Kaunti ndogo ya Embakasi James Wanyoike akisema kwamba shughuli za uokoaji huenda zikakamilika kesho.

Idadi ya watu walioaga dunia katika tukio hilo pia ilipanda hadi watu saba huku familia nyingi zikisimulia wasiwasi wao kuhusu kutoweka kwa wapendwa wao

“Bado ninasubiri watoto wangu waokolewe na ninaomba wapatikane wakiwa hai. Ninawapenda sana,” akasema Bi Venny Gechemba, mama wa watoto wawili.

Akilengwalengwa na machozi, Bi Gachemba anakumbuka kwa masikitiko namna wanawe Frank Kerosi, 11 na Ezra Kerosi, 6 walivyoondoka nyumbani na mpwa wao Eugene Momanyi lakini hawakuonekana tena.

“Waliondoka asubuhi wakiniambia wanaenda kumtembelea shangazi na wangerejea kupata staftahi lakini hawakuonekana tena. Niliendelea kulala lakini nikaamshwa na kelele kutoka nje,” akasimulia.

Aliendelea kusimulia kwamba aliamka na kuelekea kwa dadaye karibu na jengo lililoporomoka kuangalia kama watoto wake walikuwa salama.

“Nilielekea moja kwa moja kwa nyumba ya dadangu ambako watoto hao walikuwa wakienda lakini sikuwapata. Alinieleza hawakuwa wameenda kwake,” akaongeza.

Alipigwa na butwaa baada ya kuwatafuta hadi saa tano mchana siku hiyo, alipoelezwa na wavulana waliokuwa na watoto wake kwamba walikuwa wamekwama ndani ya vifusi hivyo. Wavulana hao walikuwa wameokolewa kutoka kwa jengo hilo.

Kulingana na dadaye Diana Bosibori ambaye huishi na Bw Ezra, mtoto wa marehemu wifi yake, watoto hao watatu walikuwa wakicheza kabla ya jengo hilo kuporomoka.

Kulingana na Bw Wanyoike, watu 35 wameokolewa kutoka kwenye jengo hilo huku miili miwili ikiondolewa na wengine wawili wakiaga dunia hospitalini.

“Mnamo Jumamosi mwanamume mmoja na mwingine wa kike waliokolewa na kupelekwa katika hospitali ya Kenyatta wanakoendelea kupata matibabu.