Kimataifa

Uongo aliotumia mama wa miaka 62 kupata mimba

November 14th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

MWANAMKE wa miaka 62 amekiri kuwa alihadaa madaktari kuhusu umri wake kwa kujipunguzia miaka 12 ili wakubali kumpa matibabu ya uzazi, ndipo akapata mtoto wake wa kitinda mimba.

Bi Lina Alvarez alieleza madaktari kuwa alikuwa na miaka 50, lakini wakajua ukweli baadaye tu baada ya kusoma habari zake kwenye vyombo vya habari.

Mama huyo kutoka Jiji la Lugo, Kaskazini-Magharibi mwa Uhispania alisema kuwa “madaktari walifahamu kupitia vyombo vya habari lakini hawangetunyima haki ya kuwa wazazi.

“Kwa zaidi ya miaka 10 nilikuwa nikitafuta mtu ambaye angeniwezesha kupata watoto Zaidi na sikupata yeyote hadi nilipohadaa kuhusu umri wangu,” akasema.

Mama huyo tayari ana mtoto mwanaume wa miaka 29, japo ana matatizo ya akili na mwingine wa miaka 10 ambaye kama huyo kitinda mimba alizaliwa kwa usaidizi wa teknolojia ya AI.

Sasa anasema kuwa mtoto wake wa mwisho, Linita, ambaye ana miaka miwili amempa “miaka miwili ya furaha Zaidi maishani.”

Anasema kuwa sasa anajiona kama mtetezi wa kina mama ambao licha ya uzee wangependa kuwa wazazi.

“Wanawake wengi wanapenda kuwa kina mama lakini hawapewi fursa hiyo,” akasema.

Mwanamke huyo hata hivyo yuko katika vita vya kisheria na idara ya afya ya Uhispania, ambayo anailaumu kwa huduma mbovu ambazo zilimpelekea kuzaa mtoto mwenye matatizo ya akili miaka 29 iliyopita.

Hakuna umri uliowekwa kuwa ambao mama anaweza kupewa huduma ya kujifungua ya AI Uhispania, japo idara ya afya nchi hiyo hupendekeza umri wa miaka 50, jambo ambalo lilimpelekea mama huyo kushusha umri.

Hata hivyo, baadhi ya watu wamemkashifu kwa hatua aliyofanya.

Lakini Bi Lina amedai kuwa mwanawe Linita ni mtoto mcheshi, mwenye afya bora na anayepokea mapenzi na ulezi anaostahili.