Siasa

Uongozi wa Joho wazua zogo bungeni

September 14th, 2020 2 min read

Na WINNIE ATIENO

WAWAKILISHI wa wadi katika Bunge la Kaunti ya Mombasa wametofautiana kuhusu wajibu wa Gavana Hassan Joho, huku baadhi wakikiri ni watu wake wa mkono.

Baadhi ya madiwani hao wamedai hawana uhuru wa kujadili hoja yoyote bila ya ruhusa ya Gavana Joho, ambapo wenzao walioteuliwa wamekuwa wakipitisha hoja au mswada unapopendekezwa na serikali ya kaunti hiyo bila kuidadisi.

“Sipendi ukandamizaji wa wanyonge. Kamati za bunge letu zinateuliwa kulingana na wale wanaotii amri ya bwana mkubwa. Sioni haya kuwaambia ukweli,” alidai diwani wa Kipevu, Bi Faith Mwende.

Alitoa mfano wa diwani wa Kongowea, Bw Abrary Mohammed Omar ambaye alikuwa naibu mwenyekiti wa kamati ya bunge inayosimamia ardhi lakini akatimuliwa.

“Ukisema kitu tofauti na wenye mji unang’atuliwa kutoka kamati za bunge. Nitakuwa nawaambia ukweli. Wenyeviti wote wanaimba wimbo wa Joho. Ninasikitikia sana bunge letu. Tuombe Mungu kwa miujiza lakini hamuwezi kupata haki bungeni,” aliongeza.

Diwani wa Freretown, Bw Charles Kitula aliwataka wakazi, hasa wafanyabiashara, wasusie kulipa ushuru hadi pale Bw Joho atakapowaeleza namna alivyotumia fedha za ugatuzi.

Diwani huyo ambaye alitimuliwa kutoka kwawadhifa wa Kiranja wa Wengi, alisema kosa lake kubwa ni kuuliza maswali magumu kuhusu ufujaji wa fedha.

“Ripoti ya mkaguzi mkuu wa hesabu na matumizi ya fedha za umma ilipotoka, niliona dosari katika kaunti yetu ya Mombasa. Kati ya 2013 na Machi 2020, serikali yetu imetumia Sh15 bilioni kwa maendeleo. Nina stakabadhi zote za kuthibitisha ninayoyasema. Haya maendeleo yako wapi?” akauliza Bw Kitula.

Lakini kiongozi wa vijana wa ODM tawi la Mombasa, Bw Moses Aran alimtetea Gavana akisema haingilii bunge hilo.

“ODM ina idadi kubwa ya wawakilishi wa wodi bungeni na hatufai kuonewa gere wala kulaumiwa kutokana na hilo. Bunge linaendeshwa na idadi ya waliowengi. Kati ya wawakilishi 42 wa bunge letu, mbona ni wanne tu ambao wanapiga kelele. Niliteuliwa na ODM na lazima niwe mwaminifu kwa chama,” alisema.

Bw Aran alisema Bw Joho hajawahi kuwashurutisha wala kuwaita mkutanoni ili wamuunge mkono kwenye maswala yake katika bunge.

“Sisi kama wabunge wateule 12, tumekuwa katika mstari wa mbele kutekeleza wajibu wetu kwa mujibu wa sharia.

Madiwani 27 walichaguliwa na wananchi kupitia chama cha ODM, mmoja anatoka Wiper, Ford Kenya na mwingine alikuwa mgombea huru. Bw Kitula na wenzake ni watu wa maslahi,” alisema Bw Aran.

Spika wa bunge la Mombasa, Bw Aharub Khatri alikanusha madai hayo akisema haongozi wanaopiga muhuri kwenye uongozi wa bunge hilo.

“Haya ni masuala ya kisiasa, hayanihusu. Mimi sina kura wala siko kwenye kamati za bunge. Kazi yangu ni kama jaji na kutoa uamuzi, huwa sipendelei upande wowote,” akasema.

Hata hivyo wawakilishi wa wodi teule wakiongozwa na Bi Fatma Kushe walikiri kuwa wao ni wapiga muhuri wa Bw Joho na chama cha ODM.

“Niliteuliwa na Gavana Joho kupitia ODM ambaye ni naibu kinara wa chama hicho. Siwezi kwenda kinyume na ODM wala Bw Joho. Bw Kitula alichaguliwa kupitia ODM kama yeye ni mwanamume kweli ajiuzulu na agombee kiti chake kupitia chama cha hasla. Alikuwa kiranja wa bunge, alitekeleza mangapi? Tunajua hao wasaliti wanatumika na wapinzani wetu kuzua vurugu bungeni,” alidai Bi Kushe.