Habari

Uopoaji: Wapigambizi sasa kuweka zingatio kwa sehemu ya umbali wa mita 300 baharini

October 9th, 2019 2 min read

Na MISHI GONGO

SHUGHULI ya kutafuta gari na kuopoa miili ya mwanamke na mwanawe waliozama Septemba 29, 2019, katika Bahari Hindi inaelekea kufikia sehemu iliyosalia ya umbali wa mita 300 pekee kati ya 1.2 kilomita ambazo timu ya wapigambizi ilikuwa imetambua kuwa na uwezekano wa kuwepo gari.

Kanali wa kikosi cha jeshi la wanamaji nchini, Lawrence Gituma, amesema zimesalia sehemu nne pekee zenye upana wa mita 300.

Amesema picha walizopiga katika sehemu hizo zilionyesha utandu wa tope la mita 1.5 na ishara ya chombo ambacho si kawaida kuwa baharini.

“Tuna matumaini ya kukamamilisha operesheni hii wakati wowote kutoka sasa,” akasema Kanali Gituma.

Ameeleza walifanikiwa kufikia hapo kwa kutumia kifaa maalum kilichonunuliwa na serikali – three beam system – chenye uwezo wa kuona katika sakafu ya bahari kwa mfumo wa 3D na hivyo kutoa picha halisi.

“Tuna matumaini kuwa sehemu mojawapo kati ya hizi, kutakuwa na uwezekano wa kuwa na gari lililozama kufuatia ishara ya mchanga wa sehemu hiyo umesumbuliwa na chombo ambacho si cha baharini,” akasema.

Aidha amesema wanasubiri kamera inayoendeshwa na rimokonto iliyo na uwezo mkubwa wa kuona katika sakafu ya bahari ambayo itatumika kuthibitisha chombo wanachokidhania kuwa gari la mwanamke kabla ya kutuma wapigambizi.

“Wapigambizi binafsi walioletwa na familia na wale waliokodishwa na serikali watashirikiana kuhakikisha shughuli hiyo inaendelea vizuri,” amesema.

Teknolojia

Kanali huyo amekuwa akiwataarifu wanahabari jinsi uopoaji unavyoendelea akisema kwa sasa wanatumia teknolojia zaidi ili kuharakisha shughuli ya kupata miili ya Bi Miriam Kighenda na mwanawe Amanda Mutheu waliozama baharini wakielekea Mombasa kutoka Kaunti ya Kwale.

Kanali Gituma amesema teknolojia wanayotumia kwa sasa imewawezesha kutafuta sehemu kubwa zaidi walizokuwa wametambua awali kuwa na uwezekano wa kuwa na gari.

“Tulichelewa kwa sababu tulikosa vifaa, lakini sasa hivi tumepata vifaa na tunatarajia vingine na tuna imani ya kukamilisha shughuli hii karibuni,” akasema.

Jumanne, mkurugenzi mkuu wa shirika la huduma za feri Bw Bakari Gowa alisema shughuli hiyo lililemaa kwa muda wakisubiri vifaa vitakavyowawezesha kuona sakafu ya bahari.

Alieleza kuwa ni wapigambizi wa familia pekee waliokuwa wakiendeleza operesheni hiyo lakini kufikia mchana waliungwa na wenzao katika kutafuta miili.

Mwenyekiti wa shirika la huduma za feri Dan Mwazo aliwapongeza wote wanaoendeleza shughuli za uopoaji akisema kuna matumaini ya kukamilika shughuli hiyo wakati wowote.